Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amefanya ziara ya kikazi Novemba 14, 2024, mkoani Mtwara kwa lengo la kukutana na wadau mbalimbali wa sheria na kuimarisha utoaji wa huduma za sheria kwa wananchi wa mkoa huo.
Akiwa Mtwara, Johari amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, kwa ajili ya kujitambulisha rasmi na kueleza malengo ya ziara yake. Ziara hiyo ni ya kwanza tangu ateuliwe na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mkuu wa Mkoa, Kanali Sawala, amemweleza Johari kuwa mkoa huo uko salama na serikali inaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha wananchi wanabaki salama na amani inadumishwa.

Akizungumzia lengo la ziara yake, Johari ameeleza kuwa ni kutembelea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kanda ya Mtwara na kukutana na watendaji wa ofisi hiyo kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za kisheria kwa wananchi.
“Mkoa wa Mtwara ni mkubwa na una shughuli nyingi za kiuchumi, hivyo ni muhimu kuwa na mawasiliano ya karibu kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, ofisi ya Mkuu wa Mkoa, na wananchi,” amesema Johari.
Ameongeza kuwa ziara hiyo inalenga kuimarisha utoaji wa huduma za sheria kwa maeneo mbalimbali nchini, akisisitiza umuhimu wa kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Katika ziara hiyo, Mwanasheria Mkuu pia ametembelea eneo linalopangwa kujengwa jengo la Ofisi za Kanda, pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mtwara, iliyopo kwenye jengo la Chama cha Walimu Mkoa wa Mtwara.
Ziara hii inatarajiwa kuleta mwamko mpya katika ushirikiano kati ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu na wadau wa sheria mkoani Mtwara, kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati na kwa ufanisi.