Mwanahabari mmoja wa Italia aitwaye Giulia Cortese ameagizwa kumlipa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Giorgia Meloni fidia ya €5,000 (£4,210) kutokana na machapisho ya mitandao ya kijamii yanayodhihaki urefu wake
Taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa shirika la habari la kimataifa la Uingereza (BBC) mapema leo, Ijumaa Julai 19.2024 imeeleza kuwa katika maamuzi yake Mahakama imeona jumbe mbili za Giulia Cortese katika mtandao wa kijamii wa ‘X’ (twitter), ambapo licha ya adhabu hiyo pia mwanahabari huyo ametakiwa kulipa faini nyingine ya €1,200 inayotokana na kuchafua jina Waziri mkuu, ambapo kwa mujibu wa Mahakama imeeleza kuwa machapisho ya mwanahabari huyo kwenye mitandao yake binafsi ya kijamii yanalenga ‘kumuaibisha’ Waziri Mkuu huyo kwa jamii kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kwa sababu ya mwili wake
Katika machapisho yake mwanahabari huyo Cortese alimtaja Waziri Mkuu Meloni kama ‘mwanamke mdogo’ sambamba na kwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa ‘hatamani kuonana na mtu wa aina hiyo kwenye maisha yake’
Akizungumzia maamuzi hayo ya Mahakama Cortese amekosoa vikali serikali ya Italia kwa kile alichosema kuwa ina tatizo kubwa la uhuru wa kujieleza na kwamba uhuru wa waandishi wa habari uko shakani nchini humo
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa wawili hao waligombana kwa mara ya kwanza mnamo Oktoba 2021, wakati chama cha Meloni chenye msimamo wa mrengo wa kulia cha Brothers of Italy kingali bado katika upinzani, na hiyo ilitokana na ukweli kwamba Cortese alichapisha picha ya dhihaka ya Meloni kwenye X, iliyoonesha kiongozi huyo wa upinzani wakati huo (sasa Waziri Mkuu) akiwa amesimama huku pembeni yake ikipachikwa picha ya dikteta wa kifashisti Benito Mussolin, chapisho ambalo lilitengeneza mjadala mkubwa hasi nchini humo.