Latest Posts

MWANZA YAZINDUA KAMPENI YA MAZOEZI KUWAOKOA WATUMISHI WA UMMA DHIDI YA KISUKARI, SHINIKIZO LA DAMU

Mkoa wa Mwanza umeanzisha kampeni ya watumishi wa umma kufanya mazoezi ya viungo kwa lazima kila jumamosi ya tatu ya mwezi ili kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa tishio kwa wafanyakazi hao.

Kampeni hiyo ya matembezi ya mazoezi ya viungo kwa watumishi wa mkoa wa Mwanza imezinduliwa Jumamosi Januari 18, 2024, ambapo watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na jeshi la polisi wametembea na kukimbia kilometa tano.

Akizindua kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Said Mtanda, Katibu tawala msaidizi- Miundombinu, Chagu Ng’oma amesema katika kipindi cha miaka mitano magonjwa yasiyoambukiza yameongezeka kwa asilimia 65.5 kutoka wagonjwa 149,130 mwaka 2020 hadi 224,190 mwaka 2024.

Amesema kupitia mazoezi ya viungo, mtindo wa maisha na ulaji unaofaa unaweza kuzuia magonjwa ya moyo na kisukari kwa asilimia 80 na saratani kwa asilimia 50, huku akisisitiza kuwa magonjwa hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza ufanisi wa utendaji kazi katika utumishi wa umma.

“Pamoja na jitihada za serikali za kutafuta njia mbalimbali za kudumisha afya za watumishi tatizo la magonjwa sugu yasiyoambukiza limebainika kuwa linaathiri afya za watumishi kwa kiwango kikubwa ikiwamo kupungua kwa nguvu kazi kunakosababishwa na vifo, kuongezeka kwa gharama za matibabu na kupungua kwa tija kazini, hivyo, kuathiri ukuaji wa pato la taifa,” amesema Ng’oma.

Ameongeza kuwa; “Mbinu za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza zinajulikana na zipo ndani ya uwezo wetu wa watumishi kwa kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwa ni pamoja na ulaji unaofaa, mazoezi ya mwili na kuwa na uzito usiozidi kiasi kulingana na urefu.”

Ng’oma amesema kwa kuzingatia mchango wa watumishi wa umma kwa maendeleo ya taifa, udhibiti wa magonjwa hayo mahala pa kazi unahitaji msukumo wa kipekee ili kunusuru afya zao ndiyo maana wamekuja na mazoezi hayo ambayo ni ya lazima na endelevu ili kudumisha kudumisha afya bora kwa watumishi wa umma.

Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Gabriel Mashauri amesema zaidi ya asilimia 50 ya watumishi wa umma wana viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza huku kisukari na shinikizo la damu yakiongoza.

Amesema kwa sasa tatizo la magonjwa hayo linaongezeka kwa kasi katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ikiwa pia ni kwa watu wenye kipato cha chini tofauti na ilivyozoeleka kuwa ni magonjwa ya watu wenye kipato cha juu pekee.

“Tatizo hili kwa mkoa wa Mwanza miaka mitano iliyopita limeongezeka hadi asilimia 8.1 mwaka 2024 kutoka asilimia 6.4 mwaka 2020 na magonjwa yanayoongoza ni Kisukari na Shinikizo la damu. Mpango huu utaendeleza juhudi za watumishi katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyo ambukiza,” amesema Mashauri

Naye, Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza mkoa wa Mwanza, Dkt. Saula Beichumila amesema utaratibu huo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kwa mikoa yote nchini kutokana na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza ambayo mengi yanatokana na mtindo wa maisha.

Mmoja wa watumishi wa umma aliyeshiriki mazoezi hayo, Samson Neligwa amesema utaratibu huo ni mzuri kwani watumishi wengi wanaosumbuliwa na magonjwa hayo wanapokwenda kutibiwa wanashauriwa kufanya mazoezi.

“Kufanya mazoezi ukiwa peke yako huwa kuna uzito lakini haya mazoezi ya ujumuishi yanatupa morali hata wale ambao ni wavivu watahamasika kufanya mazoezi. Nawashauri watumishi wenzetu ambao hawajahudhuria leo wajitahidi kuja awamu ijayo na kadri watakavyofanya kwa mara nyingi ndivyo watakavyopata morali ya kupenda mazoezi,” amesema Neligwa

Kwa upande wake, Josepha Tarimo, Ofisa Ugavi Mwandamizi mkoa wa Mwanza, amesema;

“Watumishi wengi tunashinda maofisini hatuna muda wa kufanya mazoezi ukishatoka ofisini unarudi nyumbani ambako unakutana na majukumu mengine, hivyo, huu utaratibu wa kufanya mazoezi Jumatatu, Jumatano na Ijumaa yanatusaidia sana kwa sisi tunaoshinda maofisini.”

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!