Mwenezi wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), Sigrada Mligo, ameendelea kufunguka kuhusu tukio lililompelekea kushambuliwa na hatimaye kulazwa hospitalini akiwa katika hali mahututi.
Kwa mujibu wa Mligo, tukio hilo lilitokea wakati wa kikao cha ndani cha wanachama wa CHADEMA kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche, baada ya mkutano wa hadhara uliofanyika siku hiyo.
Mligo anadai kuwa aliomba fursa ya kuzungumza katika kikao hicho ili kuweka wazi baadhi ya masuala kuhusu mustakabali wa chama, lakini hoja zake zilipokelewa kwa ukali. Badala ya kusikilizwa alitolewa nje.
Baada ya kufukuzwa kikaoni, anasema amemtumia Heche ujumbe wa simu akiomba kurejea ili kutoa mchango wake, lakini badala ya kufanikiwa kuingia ndani, alidai kuwa alitumiwa kundi la vijana, miongoni mwao akiwa mlinzi wa Heche, ambaye alimshambulia vibaya na kumsababishia majeraha makubwa.
“Nilijikuta nikishambuliwa bila huruma na kilio changu cha maumivu kilisababisha askari waliokuwa kwenye doria kuingilia kati na kunisaidia. Walinikimbiza katika kituo cha afya kwa ajili ya matibabu,” amesema Mligo.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Njombe kimelaani kitendo hicho, kikieleza kuwa ni uvunjifu wa amani unaoenda kinyume na misingi ya siasa za kistaarabu.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Njombe, Josaya Luoga, alizungumza hayo baada ya kumtembelea na kumjulia hali Mligo, aliyelazwa katika Hospitali ya Kibena baada ya kushambuliwa.
“Kwa kiongozi mkubwa kama Mwenezi wa BAWACHA Taifa kushambuliwa na mlinzi wa chama ni jambo la kushangaza na linasikitisha sana. Sisi tunahubiri juu ya misingi ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Uvumilivu na Ujenzi wa Demokrasia), mojawapo ikiwa ni uvumilivu na kuheshimiana,” amesema Luoga.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe limeeleza kuwa linaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo huku jitihada za kumtafuta mtuhumiwa, Noel Olevale, ambaye ni mlinzi wa chama hicho, zikiendelea.