Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara Jamali Kapende amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kusimamia urudishwaji wa 30% ya mapato yanayokusanywa kwenye vijiji ili waweze kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri hiyo.
Ameyazungumza hayo Julai 30, 2024 kwenye mkutano wa kawaida wa baraza la madiwani kuhusu kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji kwa kipindi cha robo ya nne kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Amewataka pia madiwani hao kuwasilisha miradi yote ya maendeleo bila kujali miradi ya serikali kuu.
Naye Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Abdallah Chikota amemtaka mkurugenzi huyo na timu yake kutekeleza miradi kwa wakati na kuisimamia ili iweze kuleta tija kwa wananchi pia amewapongeza kwa kuwatumikia wananchi na utendaji kazi mzuri kwani kwa kipindi hiki kero za wananchi zimepungua.
“Nikuombe mkurugenzi na timu yako, kutekeleza miradi kwa wakati na kuisimamia ili iweze kuleta tija kwa wananchi na niwapongeze kwa kuwatumikia wananchi na utendaji kazi mzuri kwani kwa kipindi hiki kero za wananchi zimepungua”, amesema Chikota.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mtwara Vijijini, Nashir Pontiya amewataka madiwani kwa kushirikiana na wananchi kutunza vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla ili wananchi waendelee kupata maji kwa uhakika na urahisi.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mhandisi Mshamu Munde amewasisitiza watendaji wa kata kuhakikisha kila kata inavuka 80% ya malengo ya ukusanyaji wa mapato na kuwataka kuwa makini kwenye upangaji wa viwango vya ukusanyaji wa mapato kulingana na hali halisi ya kata husika.