Latest Posts

MWENYEKITI UWT MBARALI: WANAWAKE WA MBARALI MGOMBEA WETU NI MMOJA

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi- CCM (UWT) Wilaya ya Mbarali, umeadhimisha miaka 48 ya CCM kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kutembelea miradi na kutoa msaada wa vitu mbalimbali hospitalini na shuleni na kuwataka wanawake na wana CCM kwa ujumla kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo katika kata ya Lugelele wilayani Mbarali, mwenyekiti wa UWT Wilaya hiyo Bi. Zabibu Nuroo, amesema wanawake wa wilaya yake wanaye mgombea mmoja tu wa ubunge katika jimbo hilo ambaye ni Mbunge wa sasa Bahati Keneth Ndingo huku akisema kwa ngazi ya taifa hakuna mjadala kwani tayari Dkt. Samia Suluhu Hassan alishapitishwa kuwa mgombea wa nafasi ya Rais baadaye Oktoba 2025.

“Niwaombe tu ndugu zangu wanawake tupendane, tushirikiane, tushikamane, tuzipende familia zetu, akina mama tusibweteke majumbani tutoke twende mashambani tukatafute ridhiki”, amesema Bi. Zabibu huku akiwapongeza wanawake kwa kufanikisha maadhimisho hayo.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mbarali, Bahati Keneth Ndingo, amewapongeza wanawake kwa kuungana kuadhimisha miaka 48 ya CCM na kueleza miradi mbalimbali inavyotekelezwa na serikali hasa miradi ya maji, barabara na huduma ya nishati (umeme) wilayani humo, nishati ambayo sasa imesalia vitongojini pekee.

Amesema wakati watu wengine wakitoa lugha mbaya au matusi wana-CCM waendelee kusema kazi zinazofanywa na CCM kwa maslahi ya wananchi na inapofika kipindi cha uchaguzi mkuu wakamchague Dkt. Samia Suluhu Hassan na wagombea wa CCM kuwa viongozi wao kwakuwa wana sera bora na zinazotekelezeka.

Pamoja na yote katika maadhimisho hayo, Mbunge wa Mbarali na umoja wa wanawake hao wilayani humo wametoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo mitungi ya gesi kwa akina mamantilie, vifaa vya masomo kwa watoto wa mahitaji maalum katika shule ya msingi Igomelo na kwa hospitali ya wilaya ya Mbarali huku pia wana-CCM wakifanya pia usafi katika kituo cha afya Rujewa.

Maadhimisho ya miaka 48 ya CCM kitaifa yanatarajiwa kufanyika Februari 05, 2025 jijini Dodoma na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!