Latest Posts

MWILI WAKUTWA UMETELEKEZWA DODOMA, MWINGINE AUAWA KIKATILI NA KUFUNGWA KAMA MZIGO

Matukio mawili yaliyoacha simanzi yametokea Mtaa wa Chinyika kata ya Mkonze Jijini Dodoma baada ya miili ya watu wawili kukutwa ikiwa imetelekezwa katika maeneo mawili tofauti ya mtaa.

Tukio la kwanza ni mwili wa dada (35) aliyetambulika kwa jina la Alice Yaredi kukutwa ukiwa umetelekezwa mlangoni nje ya nyumbani kwao alfajiri ya tarehe 22 Julai, 2024 huku ukiwa hauna jeraha la aina yoyote.

Mwenyekiti wa mtaa wa Chinyika Aloyce Athanas amesema dada huyo mwenye watoto wanne hakuwa akiishi kwa kutulia nyumbani na badala yake amekuwa ni mtu wa kuondokaondoka kutafuta maisha sehemu nyingine bila kutoa taarifa.

Kwa upande wao ndugu wa marehemu wameeleza kushtushwa na tukio hilo wakisema hawafahamu chanzo cha kifo chake huku ikiwa ni takribani wiki tatu za yeye kutokuonekana nyumbani na hata mawasiliano ya simu alikuwa akiwasiliana na majirani wa pembeni ambao ni marafiki zao.

Mama wa Marehemu Bibi Karen Yaredi amesema mtoto wake alipoondoka kwa mara ya mwisho hakuwahi kumpigia simu na hata pesa za matumizi alikuwa akituma kwa majirani.

“Sijui mtoto wangu kama kapigwa au kafanywa nini maana hakuwa hata na jeraha, tumekuta mwili tu ukiwa umelazwa nje kama mzigo” Ameeleza Bi. Karen katika hali ya kusikitika.

Akieleza namna ilivyokuwa mama huyo amesema aliitwa na mjukuu wake ambaye ndiye alikuwa wa kwanza kuuona mwili huo na kisha kumwita bibi yake baada ya kumuona akachukua hatua za kumuita mwenyekiti na majirani huku dada wa marehemu aitwaye Gema Yaredi akisema waliingiwa na taharuki walipogundua kifo cha ndugu yake.

“Mimi nilikuwa nimelala ile saa 11 asubuhi nikasikia watu wanaongeaongea, kuna mtoto wa dada yangu akawa ameshaamka asubuhi ili akachukue vitu vya gengeni alipofungua mlango akamkuta mama mdogo wake akaanza kumuita mbona umelala hapa nje, lakini ikawa kimya ndipo akaja kutuita tulipokwenda kumuita wala hakuitika na alikuwa amelala akiwa hana hata nguo, nasi tukamuita wala haitiki ndipo tukaanza kupiga mayowe watu wakaja kumwangalia na kusema huyu ameshakufa tayari” Amesema Dada wa marehemu.

Naye rafiki wa marehemu aitwaye Mwancheni amesema mara ya mwisho alimuona Alice akiwa anaelekea mahali na kumwita kisha kumuuliza anaelekea wapi ndipo akamjibu kuna sehemu anaelekea ana haraka hivyo atamcheki kwenye simu.

“Baada ya kuachana pale ilikuwa tarehe 01 mwezi wa saba, siku ya pili akanipigia na kuniuliza niko wapi, nikamjibu nipo nyumbani akasema nataka nikutumie hela hapo umpe mwanangu akirudi kutoka shule asiteseke atanunua hata chips, nilipoendelea kuwasiliana naye nikamuuliza sasa wewe mbona hurudi huko una mishe gani akasema mi nipo tu” Ameeleza rafiki wa marehemu.

Tukio lingine ni la tarehe 21 Julai, 2024 katika mtaa huohuo, linaelezwa kuwa la kikatili baada ya kukutwa mwili wa dada asiyejulikana kukutwa umetupwa na kuwekwa kwenye mfuko na kufungwa na maboksi.

Mwenyekiti wa mtaa huo ameeleza kuwa mwili huo ulikutwa ukiwa umefungwafungwa mithili ya mzigo wa nguo za mitumba na kutupwa kichakani ng’ambo ya mto.

“Jana Saa kumi jioni mzee mmoja alikuwa ametoka kuchunga ng’ ombe zake porini ndipo akakutana na ule mzigo ukiwa umetupwa, yule mzee alipouangalia ule mzigo akajua labda leo nimejiokotea dodo huku kuna mali fulani, akamwita mwenzake njoo tusaidiane kufungua huu mzigo tuangalie kuna nini, baada ya kufungua wakaanza kuona upande wa miguu wakakutana na nyayo za binti ndipo wote pale wakachanganyikiwa na kuanza kupiga kelele, ndipo tukaenda pale na kuita Jeshi la Polisi likaja kuangalia ule mwili na kuuchukua” Ameeleza Mwenyekiti.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma limeahidi kuwa litatoa taarifa rasmi siku ya kesho kuhusiana na matukio hayo yaliyozua taharuki kwenye jamii.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!