Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, amesema Jeshi la Polisi halitavumilia Askari wanaojihusisha na majukumu yasiyo yao, ikiwemo kujivisha Vyeo vya Taasisi nyingine kwa lengo la kujipatia rushwa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo katika eneo la Kariakoo, Muliro amesema tayari ametoa maelekezo ya kiutendaji kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala pamoja na OCD wa eneo husika, kuhakikisha Askari wanajikita katika majukumu yao ya msingi.
“Nimetoa maelekezo ya kiutendaji kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala na OCD wa eneo hili kwamba lazima tujikite kwenye majukumu yetu ya msingi, na tusiache majukumu hayo tukafanya ya watu wengine. Endapo kuna taarifa zinazohusiana na uvunjifu wa Sheria, sisi kama Polisi tunafanya uchunguzi na kushirikiana na Mamlaka husika,” amesema Muliro.
Aidha, ameongeza kuwa Jeshi la Polisi halipaswi kuingilia Majukumu ya Taasisi nyingine za Serikali kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
“Sisi tusijifanye ndio TBS, tusijifanye ndio TRA, wala Mkemia Mkuu wa Serikali. Hayo tayari tulishayaelekeza. Askari wachache wanaokiuka maelekezo haya hufanya hivyo si kwa nia njema, bali kwa maslahi binafsi,” amesema.
Sanjari, na hayo Muliro amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vya rushwa, na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya Askari watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo, ili kulinda heshima na uadilifu wa Jeshi hilo.