News Njombe.
Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa amemaliza mgogoro wa kiwanja uliodumu zaidi ya miaka nane baina ya mzee Michael Mwenda na serikali ya Mtaa wa Mgendela mjini Njombe na kumrejeshea eneo lake mzee Mwenda aweze kuliendeleza.
Awali mzee Mwenda mbele ya Mkuu wa Wilaya amesema alitoa sehemu ya eneo lake bure kujenga ofisi ya mtaa huku aneo jingine akitoa kwa ajili ya ujenzi wa kanisa lakini alishangaa baadaye kuona viongozi wa mtaa wakimzuia alipohitaji kuendeleza sehemu ya eneo lake wakidai kuwa eneo hilo ni mali ya serikali ya mtaa.
“Ushahidi mwingi tumeuleta lakini tunasumbuliwa, tumetoa eneo kwa ajili ya kanisa bure, tumetoa eneo la kujenga ofisi bure lakini tumekuja kurasimisha eneo letu lilobaki tumezuiwa na tulikubaliana wanapojenga ofisi basi huku mbele waache, ni kwangu sasa nimewaambia vijana pelekeni mawe pale kiwanja kilichobaki mjenge kabanda anazuiwa kwamba ni mali ya ofisi, mali ya ofisi tangu lini?” Alihoji mzee Mwenda.
Hata hivyo mara baada ya kuwasikiliza wananchi wa mtaa huo, viongozi wastaafu wa mtaa waliopo madarakani, pamoja na familia, DC Kissa Kasongwa amejiridhisha kuwa eneo hilo ni mali ya mzee Mwenda na kuagiza Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe inatoa hati kwa ajili ya eneo la ofisi pamoja na eneo lililobaki la mzee lililokuwa limezuiwa.