Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Tanzania Bara Mussa Mwakitinya amewasihi Vijana wote nchini kuepuka kutumika kubeba ajenda za wanasiasa ‘zisizokua njema’ katika nchi.
Mwakitinya ametoa nasaha hiyo wakati wa zoezi la ufungaji wa kambi ya mafunzo ya vijana wa CCM Songea Mjini hivi karibuni akiwataka kujitambua kuwa wao ni nguvu kazi ya taifa.
“Kamwe msikubali kubeba ajenda za wanasiasa uchwara mkaingia barabarani kuandamana, kumbukeni dhamana ya maisha yenu ipo mikononi mwenu, kesho ya vijana ni kubwa sana, kamwe msikubali hawa wanasiasa ambao wamekosa kazi za kufanya kuwabebesha ajenda zao zisizokua njema katika nchi yetu”, ameeleza Mwakitinya.
Aidha amewasihi vijana wote nchini kutunza afya dhidi ya magonjwa kwani wao ni nguvu kazi ya taifa na jamii inategemea katika kukuza na kulinda uchumi wa taifa lao huku akiwakumbusha kuwa mapinduzi ya kiuchumi yanaletwa na watu wenye siha njema.
“Ndugu zangu vijana afya ndiyo msingi wa kufanya kazi, tujiepushe na michepuko tubaki njia kuu na tutumie kinga kujilinda dhidi ya magonjwa afya zetu ziwe imara. Taifa hili linatutegemea” ameeleza Mwakitinya.
Katika hatua nyingine Mwakitinya amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameifungua nchi kwa kufanya uwekezaji mkubwa wa miradi inayowanufaisha vijana moja kwa moja hivyo ni muhimu kwa vijana kumuunga mkono.
“Ni jukumu letu kama vijana ambao ni wanufaika namba moja wa uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kumuunga mkono ifikapo 2025 na kwenye hili sisi Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi tulishakubaliana fomu ni moja tu na tulishaazimia kwenda kumchukulia fomu ya kuomba ridhaa 2025”, ameeleza Mwakitinya.