Naibu Msajili wa vyama vya siasa nchini Mohammed Ali Ahmed amesema sheria na kanuni za maadili ya vyama vya siasa zinaendelea kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kuweka usawa wa kijinsia pamoja na kukuza uwajibikaji na kuzuia unyanyasaji dhidi ya wanawake ili waweza kushiriki kikamilifu katika siasa na demokrasia nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Msajili wa vyama vya siasa, Afisa sheria Mwandamizi kutoka ofisi hiyo Abdulrazak Ali kwenye mkutano wa tathmini iliyoangalia vikwazo vinavyowakwaza wanawake katika kugombea na kushiriki masuala ya kisiasa uliofanyika ukumbi wa ZURA Maisara mjini Unguja, ambao ukiwashirikisha wadau mbalimbali kutoka taasisi za Serikali, vyama vya siasa, Asasi za kiraia, wanaharakati na viongozi wa dini.
Kwa mujibu wa Ali, sheria na kanuni zinazoendelea kufanyiwa marekebisho ni pamoja na Sheria ya Vyama vya Siasa (2019) na Kanuni za maadili ya vyama vya siasa na kanuni nyingine, ambapo marekebisho hayo yatakapokamilika yanatarajiwa kuondoa unyanyasaji kwa wanawake katika kushiriki masuala ya kisiasa.
Aidha amesisitiza kuwa usawa wa kijinsia ni jambo lisilopingika, hivyo ni muhimu kwa vyama vya siasa kuzingatia hilo kwa kuandaa miongozo imara itakayosimamia maadili na kukemea vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake, sambamba na kuunga mkono wanasiasa wanawake, wagombea, wapiga kura ambao wanaweza kukabili vitisho, vurugu, kashfa na dhihaka kutokana na jinsia zao katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Mapema akimkaribisha Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, na Watoto, Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar Dkt. Mzuri Issa amesema kumekuwa na malalamiko ya wanawake kudhalilishwa wakiwa katika harakati za ushiriki wao katika siasa na hakuna mifumo mizuri ya kuripoti matukio hayo na upatikanaji wa haki.
Naye Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto Zanzibar Anna Athanas Paul, amesema Wizara hiyo imeandaa mikakati maalumu ikiwamo kutoa mafunzo, nyenzo na programu za ushauri ili kusaidia wagombea wanawake.
Tathmini ya vikwazo kwa wanawake katika kushiriki kwenye siasa na demokrasia imefanywa na TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Kitaifa la Kidemokrasia (NDI) na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).