Latest Posts

NAIBU WAZIRI SANGU AKERWA NA MAAFISA UTUMISHI KUTOA USHAURI KUWAFURAHISHA WAKUU

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deus Sangu ameonya tabia ya baadhi ya Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala kutoa ushauri kwa lengo la kuwafurahisha wakuu wao badala ya kusimamia miongozo ya kazi zao hali inayopelekea ushauri huo kuwaumiza baadhi ya watumishi.

Amesema tabia hiyo ya kujipendekeza imejengeka miongoni mwa Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala hao ya kutaka kuonekana wao ni wema na wasiotaka kuwakwaza Wakuu wao muda wote

Sangu ametoa kauli hiyo kwenye kikao kazi cha Watumishi wa Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa mara baada ya kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi, ikiwa ni ziara ya kwanza kuzungumza na watumishi tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Amesema tabia hiyo imewaumiza watumishi wengi kwani muda mwingi hutoa ushauri ambao ni kinyume cha haki na wajibu wa utumishi.

Katika hatua nyingine Sangu amezitaka mamlaka za ajira na nidhamu kusimamia haki na stahiki zote za watumishi huku akizionya kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.

Amesema ni jambo la aibu kuona watumishi waliostaafu wakianza kuhangaika kufuatilia taarifa zao ilhali kuna watu wanalipwa mshahara kwa ajili ya kazi hiyo.

Amesema kitendo cha watumishi wastaafu kuanza safari ya kuhangaika ya nenda rudi katika kufuatilia taarifa zao kana kwamba wao ndio waliojiajiri kinaleta taswira mbaya kuwa thamani na umuhimu wa mtumishi wa umma ipo tu pale ambapo mtumishi huyo akiwa bado hawajastaafu. Hivyo, Sangu ameagiza taarifa za watumishi ziandaliwe mapema ili anapofikia umri wa kustaafu ziwe zimekamilishwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!