Latest Posts

NAIBU WAZIRI SANGU: TAKUKURU JIPANGENI KUDHIBITI RUSHWA UCHAGUZI 2025

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonesha wazi dhamira ya kupambana na rushwa kwa vitendo, kwa kuiwezesha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa rasilimali fedha na watumishi.

Sangu ametoa kauli hiyo, Desemba 16, 2024, jijini Arusha, wakati Makamu wa Rais, Philip Mpango, alipomwakilisha Rais Samia katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2024 wa Viongozi wa TAKUKURU.

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia, TAKUKURU imepatiwa vibali vya kuajiri watumishi wapya 980, rasilimali fedha, magari, samani, na kompyuta. Aidha, taasisi hiyo imewezeshwa ujenzi wa ofisi mpya katika wilaya, mikoa, na Makao Makuu yake.

Sangu ameeleza kuwa hatua hizo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020, na zimeongeza ufanisi wa TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa.

Naibu Waziri Sangu pia ameiagiza TAKUKURU kujipanga vyema kudhibiti vitendo vya rushwa katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, na Madiwani mwaka 2025.

“Rushwa ni adui wa maendeleo na tukiacha vitendo vya rushwa vitamalaki katika uchaguzi tutapata viongozi wasiokuwa waadilifu na malengo ya Serikali ya kuleta ustawi wa wananchi hayatafanikiwa” amesisitiza Sangu.

Sangu ametoa rai kwa jamii kutokukubali kushiriki vitendo vya rushwa katika uchaguzi ujao, akihimiza ushirikiano wa kila mmoja kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa huru na haki.

“Kila mmoja wetu akikataa kushiriki vitendo vya rushwa, tutakuwa tumeshiriki kuijenga Tanzania yenye maendeleo,” amesema.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!