Latest Posts

NAIBU WAZIRI WA MAJI AMTAKA MKANDARASI WA MIJI 28 KUONGEZA KASI YA UJENZI GEITA

Na Joel Maduka, Geita.

Naibu Waziri wa maji Mhandisi Kundo Mathew, amemtaka mkandarasi wa kampuni ya AFCONS Infrastructure Ltd anayetekeleza mradi wa miji 28 mkoani Geita kuhakikisha anaongeza nguvu kazi ya mradi huo uweze kukamilika ndani ya muda husika kama ilivyopangwa.

Mhandisi Kundo amesema hayo wakati alipotembelea mradi wa kusambaza maji ambao utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 124 unaojengwa kwenye Kata ya Senga wilayani Geita ambapo amesema lengo la ziara yake ni kuona hatua iliyofikiwa katika utekelezaji sambamba na kutoa maelekezo kwa wakati ili wananchi wapate huduma.

“Nimegundua kwamba zaidi ya asilimia 45 ya muda umeshatumika huku utekelezaji ukiwa ni asilimia 18, ukiangalia muda na utelezaji wako vipo tofauti, kwa maana ya kwamba tupo nyuma ya muda. Miradi hii ya miji 28 inatekelezwa katika Wilaya ya Geita na Chato, niseme tu ukweli sijaridhishwa na utekelezaji wa mradi huu pamoja na kwamba kuna sehemu zimejengwa lakini nimuelekeze mkandarasi aongeze kasi ya utendaji kazi” Amesema Mhandisi Kundo.

Mhandisi Kundo amemtaka mkandarasi kuongeza idadi ya watumishi, wakiwemo wahandisi wa ndani na kuhakikisha kila ambaye anakuja kwenye eneo la mradi anakuwa na mkataba wa kisheria ambao utamlinda mwekezaji na mwajiriwa.

“Nina uhakika haya ambayo nimetoa kama maagizo wakiyazingatia tutarajie kupata maji kwenye baadhi ya vijiji mwezi wa sita mwakani” Amesisitiza Mhandisi Kundo.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Geita (GEUWASA), Mhandisi Frank Changawa amesema matarajio waliyonayo kufikia Disemba 2025 mradi huo utakuwa umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wataanza kutumia maji safi na salama.

“Waziri tunamshukuru kwa ziara yake tunaamini amejionea baadhi ya miradi na ametoa maelekezo kwenye miradi ambapo sisi jukumu letu ni kukubali maagizo yote ambayo ametoa na kuhakikisha tunayatekeleza” Alisema Mhandisi Changawa.

Mradi huo wa maji ukikamilika unatarajiwa kuzalisha lita milioni 45 na kusambaza maji kwenye vijiji 19 katika jimbo la Geita vijijini na kusambaza maji kwenye kata zote 13 za halmashauri ya mji wa Geita.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!