
Diwani wa Kata ya Mkiwa, Stephen Petro Mtyana amesema kambi iliyowekwa na askari wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika kijiji cha Mkiwa kilichopo kata ya Mkiwa, wilaya ya Ikungi mkoani Singida yenye lengo la kuwafukuza tembo imerejesha amani na matumaini kwa wananchi wa kijiji hicho ambao wamekuwa wakisumbuliwa na wanyamapori hao kwa muda mrefu.
Stephen Mtyana ameyasema hayo Novemba 02, 2024 alipokuwa akiongea na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari katika Kijiji cha Mkiwa baada ya kutembelea kambi hiyo ya askari.
“Wanyama hawa wamekuwa wasumbufu, siku hadi siku kuanzia huko nyuma lakini kwasasa baada ya kufika kikosi hiki cha wataalamu kutoka TAWA wametusaidia kuwaondoa hapa walipo kwenye makazi yetu na kuwapeleka mbali, ilivyo bahati wametuletea ndege nyuki wanaoweza kuwafukuza tembo na kuwapeleka mbali Zaidi”, amesema Stephen.

Naye Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema kutokana na changamoto ya wanyamapori hao, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TAWA imeona umuhimu wa kuweka kambi katika kijiji cha Mkiwa ili kuhakikisha maisha na mali za wananchi wa kijiji hicho vinakuwa salama.
Aidha amesema TAWA imepeleka vikosi vitatu vya askari zaidi ya 20 vikiwa na vitendea kazi vya kutosha kukabiliana na wanyamapori hao ikiwemo magari matatu, silaha za moto, na ndege nyuki mbili ikiwemo ndege nyuki kubwa aina ya DJI Agras T30, yenye uwezo wa kubeba lita 10 za maji yenye pilipili maalumu kwa ajili ya kuwafukuza tembo.

Maganja ameomba ushirikiano kutoka kwa wananchi wa kijiji hicho na kuwataka kuondoa wasiwasi kwakuwa askari wa TAWA wamejipanga na wako timamu kuwakabili wanyamapori hao.
Kwa upande wake Afisa Uhifadhi kutoka Kanda ya Kati ya TAWA Winnie Kweka amesema awali TAWA imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali zenye lengo la kuwasaidia wananchi wa wilaya hiyo ikiwemo kuwapa elimu na mbinu za kujilinda dhidi ya athari ya wanyamapori hao.
Aidha amebainisha kuwa kijiji hicho na wilaya ya Ikungi kwa ujumla pamoja na maeneo mbalimbali ya mkoa wa Singida, yameangukia katika mfumo ikolojia wa Ruaha – Rungwa, mfumo unaotajwa kuwa na tembo wengi ambao wamekuwa wakipita katika Kijiji cha Ukiwa na kuelekea Pori la Akiba Swagaswaga kwa ajili ya kupata mahitaji yao ya msingi.

Kutokana na hali hiyo Mhifadhi Winnie Kweka ametoa wito kwa wananchi hao kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuepuka kufanya shughuli zao kwenye shoroba.