Latest Posts

NDEJEMBI: HALMASHAURI ZINUNUE MAFUTA KINGA YA WENYE UALBINO NCHINI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu Deogratius Ndejembi amezitaka Halmashauri nchini kutenga bajeti ya fedha kwa ajili ya kununua mafuta kinga dhidi ya mionzi ya jua kwa watu wenye ualbino kwa kuwa jukumu la Halmashauri za wilaya ni kuhudumia wananchi.

Ameyasema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuongeza Uelewa Kuhusu Ualbino (IAAD) ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Mailmoja wilayani Kibaha mkoani Pwani ambapo Waziri Ndejembi amewakilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge.

Amesema hayo ni maagizo ya serikali kwa halmashauri zote nchini zihakikishe zinatenga bajeti ya fedha kwa ajili ya kununua mafuta kinga dhidi ya mionzi ya jua kwa watu wenye vimelea vya ualbino.

“Halmashauri zote zihakikishe zinatenga bajeti na fedha zinapatikana, na fedha hizo zinanunua mafuta yenye kutoa kinga dhidi ya mionzi ya jua maana mnaweza kusema mmeweka kwenye bajeti lakini changamoto ni kwamba bajeti hiyo fedha haipatikani au fedha zikipatikana hazifanyi kazi ya kununua mafuta hayo” Amesema Kunenge kilichoelezwa kwenye ujumbe wa Ndejembi.

Akizungumzia ushiriki wa chaguzi za Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu, Ndejembi amewaeleza watu wenye ualbino kuwa wana haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi na akawataka kuitumia vizuri nafasi hiyo.

Katika hatua nyingine Ndejembi ameeleza kuwa serikali imeelekeza Maafisa Elimu Maalumu na Maafisa Ustawi wa Jamii wa Mikoa na Halmashauri nchini kuhakikisha wanafanya utambuzi wa watu wenye ulemavu ikiwamo watu wenye ualbino na kufanya usajili wa watu hao kwenye rejesta ya kumbukumbu za watu wenye ulemavu katika ofisi za watendaji wa mitaa na vijiji.

Awali Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TASS) Godson Mollel ameiomba serikali kuwawekea mazingira ya usalama watu wenye ualbino katika kipindi ambacho nchi inaelekea kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwishoni mwa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kwani ni wakati ambao huwa na matukio ya hatari kwa kundi hilo maalumu.

Naye Raphael Meella ambaye ni mwakilishi wa Mkuu wa jeshi la Polisi IGP Camilius Wambura amesema Jeshi la Polisi nchini limejipanga kusimamia na kulinda watu wenye ualbino ambapo tayari kuna polisi kata 3945, wakaguzi, na makamishina wa kusimamia polisi jamii ili kuhakikisha usalama wao.

Mkurugenzi Kitengo cha Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Rasheed Mafta amesema wataendelea kushirikiana na watu wenye ualbino katika mambo mbalimbali ya kijamii.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!