Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Mashariki Kusini limepiga marufuku matumizi ya eneo la dampo na machimbo ya mchanga ya eneo la Kiegeani Halmashauri ya Wilaya ya Mafia mkoani Pwani kwa kosa la kushindwa kukidhi vigezo vya utunzaji wa mazingira.
Marufuku hiyo imetolewa na Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki Kusini Lilian Kapakala akiwa wilayani humo kwenye mwendelezo wa ukaguzi wa kawaida wa kuangalia utekelezaji wa sheria za mazingira na masharti yake ikiwamo katazo la mifuko ya plastiki kutupwa kiholela kwenye ardhi.
“Halmashauri ya Wilaya ya Mafia na Wadau wa Maendeleo wa Wilaya hiyo wahakikishe kuanzia masokoni wazingatie kampeni ya katazo la mifuko ya plastiki lifanyiwe kazi na hatutaki kuona tena plastiki wilayani Mafia” Amesema Lilian.
Aidha Kapakala amesema Halmashauri ya Wilaya ya Mafia iache mara moja kutupa takataka katika maeneo ya Kiegeani na kwamba watenge eneo mahususi kwa ajili ya matumizi hayo ya dampo na machimbo ya mchanga.
Lilian amesema wamekuwa wakiangalia namna ambavyo Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 inavyotekelezwa na wadau mbalimbali ikiwamo wenye viwanda, hoteli na Halmashauri nchini huku akiwataka wasioitekeleza waizingatie sheria hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Abdul Kitungi amesema eneo hilo lilikuwa ni machimbo ya mchanga na sasa limenunuliwa na Halmashauri ya Kijiji cha Kiegeani kwa ajili ya ujenzi wa dampo la kisasa lililotengewa Shilingi milioni 400.
“Lakini litakapokuwa tayari tutawaona wataalamu hususani wataalamu wa utunzaji wa mazingira NEMC ili tuweze kushauriana nao na kushirikiana nao ili kutunza mazingira, wao wakiwa ni ni wataalamu wanaotoa maelekezo na sisi tupo tayari kuyazingatia kwa ajili ya kulinda na kutetea sheria na kanuni za utunzaji wa mazingira wa taifa letu”, alisema Kitungi.