Na Amani Hamisi Mjege,
Viongozi wa chama cha Republican cha Marekani wamesema kuwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu atawasilisha ukweli kuhusu vita dhidi ya Hamas huko Gaza atakapohutubia Bunge la Marekani Julai 24, 2024 katika ziara yake mjini Washington.
Spika wa Bunge la Marekani Mike Johnson na Kiongozi wa Wachache katika Seneti Mitch McConnell wamesema kuwa Netanyahu atazungumza katika kikao cha pamoja cha Baraza la Wawakilishi na Seneti.
“Nimeguswa sana kuwa na fursa ya kuiwakilisha Israel mbele ya Mabunge yote mawili ya Congress na kuwasilisha ukweli kuhusu vita vyetu vya haki dhidi ya wale wanaotaka kutuangamiza kwa wawakilishi wa watu wa Marekani na dunia nzima,” Amenukuliwa Netanyahu.
Ziara ya Netanyahu inakuja huku kukiwa na mvutano kati yake na Rais wa Marekani Joe Biden ambaye ameunga mkono kampeni ya Israel huko Gaza, lakini hivi karibuni amekuwa akikosoa zaidi mbinu zake na kuzuia usafirishaji wa baadhi ya mabomu. Bado haijafahamika kama Netanyahu atakutana na Biden akiwasili Marekani.
Ripoti ya shirika la habari la Reuters inaeleza kuwa uungaji mkono wa Biden kwa Israel umeibuka kama dhima ya kisiasa kwake katika kipindi ambacho Marekani inaelekea uchaguzi wa Novemba huku baadhi ya Wanademokrat na wapiga kura wakiwa na hasira kutokana na maelfu ya vifo vya raia huko Gaza.
Warepublican pia wamemkosoa Biden kwa msimamo wake kuhusu vita wakisema hafanyi vya kutosha kuisaidia Israel.
Mwezi uliopita mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai Karim Khan aliomba hati ya kukamatwa kwa kiongozi huyo wa Israel na waziri wake wa ulinzi Yoav Galant, kwa tuhuma zinazohusiana na vita.
Netanyahu alilaani hatua hiyo kwa kusema imelinganisha Israel ya kidemokrasia na kile alichokiita wauaji wa halaiki.
Hamas ilishambulia eneo la Israel Oktoba 7, 2023, na kuua karibu watu 1200 na kuwakamata mateka zaidi ya 250 kulingana na hesabu za Israel huku takriban nusu ya mateka wakiachiliwa katika mapatano ya Novemba.
Israel ilijibu mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Gaza ambayo tangu wakati huo yameua zaidi ya watu 36,000 kulingana na maafisa wa afya katika eneo hilo, ambao wanasema maelfu ya waliokufa wanahofiwa kufukiwa chini ya vifusi.