Na Amani Hamisi Mjege.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Prof. Kitila Mkumbo, ameweka wazi kuwa ana imani kubwa na kazi aliyoifanya katika jimbo lake, huku akiwatoa hofu wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi wa wilaya ya Ubungo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Prof. Mkumbo, akizungumza katika kipindi cha “Good Morning” cha Wasafi FM siku ya Jumatano Oktoba 9, 2024 amesema kuwa changamoto kubwa aliyokutana nayo alipoingia madarakani katika jimbo la Ubungo ilikuwa ni miundombinu, hasa barabara za mitaani, na kwamba juhudi za kutatua changamoto hiyo zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa.
“Nilipoingia Ubungo, tulikuwa na kilomita 5.2 tu za barabara za lami za mitaani, lakini tunapokwenda mwaka 2024, tutakuwa tumeongeza kilomita 22.4. Hii ni kazi kubwa tumeifanya, na naamini wananchi wanatuelewa. Hii ni kazi ya CCM, ni kazi ya Rais wetu, na kwa kweli tunaenda vizuri,” amesema Prof. Mkumbo.
Ameendelea kufafanua kuwa wamefanya kazi kubwa katika sekta ya afya pia, akitaja mafanikio kama kujengwa kwa hospitali ya wilaya, Kimara Baruti, na kuboreshwa kwa vituo vya afya vilivyokuwepo, ikiwa ni pamoja na kile cha kata ya Makuburi na kata ya Mabibo, ambavyo sasa vinatoa huduma za uzazi kwa kina mama.
Akizungumzia sekta ya elimu, Prof. Mkumbo amesema kuwa serikali imeongeza shule mbili za sekondari kwenye kata zilizo ndani ya jimbo lake na imeendelea kupanua na kukarabati shule za msingi zilizokuwepo.
“Kwenye huduma za elimu, tumejenga, tumeendelea kuboresha, na tumefanya kazi kubwa sana. Hakuna eneo ambalo hatujagusa, na naamini mbele ya wananchi tutakuwa na mengi ya kujivunia.” Amesema Prof. Mkumbo.
Mbali na mafanikio hayo, Prof. Mkumbo alikabiliana na swali kuhusu ushindani kutoka kwa wanachama wa vyama vya upinzani na hata ndani ya CCM katika kinyang’anyiro cha ubunge wa 2025. Ameweka wazi kuwa yeye siyo tu mwanasiasa, bali pia ni mtafiti aliyejikita katika kufanya tathmini za kina kuhusu hali ya kisiasa na maendeleo ya jimbo lake.
“Wakati naingia jimboni mwaka 2020, nilimshinda Boniface Jacob wa CHADEMA kwa asilimia 72, na yeye akapata chini ya asilimia 20. Hivyo, hakuna kitu kipya hapa. Nimekaa miaka mitano nikiwa nafanya kazi kwa bidii, na kwa kazi tulizofanya nipo imara sana. Ninawakaribisha wote tukashindane 2025.”, ameeleza Prof. Mkumbo.
Katika kuhitimisha mahojiano hayo, Prof. Mkumbo aliwaambia wananchi wa Ubungo kuwa waendelee kuwa na matumaini makubwa na yeye na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani kazi aliyoifanya yeye na serikali ni ya kupongezwa, na anaamini kuwa wananchi watatambua juhudi hizo wakati wa uchaguzi wa mwaka 2025.