Latest Posts

NTOBI AMPONGEZA MWENYEKITI MPYA WA CHADEMA LISSU, LICHA YA HISTORIA YA KUMKOSOA

Emmanuel Ntobi, kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ametoa pongezi kwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Tundu Lissu, kutokana na ushindi wake wa nafasi ya uenyekiti wa taifa.

Kupitia chapisho lake katika mtandao wa X, Ntobi pia amemshukuru Freeman Mbowe, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, kwa mchango wake mkubwa katika kukuza demokrasia ndani ya chama na taifa kwa ujumla.

“Binafsi, ni muumini wa demokrasia, na uhuru wa maoni. Uchaguzi ndani ya Chama umekamilika vema. Nampongeza sanaTundu Lissu kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Taifa. Shukrani Freeman Mbowe kwa kutoa darasa la demokrasia kwa vitendo katika chama na taifa kwa ujumla. Tuendelee na mapambano yaliyopo mbele yetu! #StrongerTogether.” Ameandika Ntobi katika ujumbe wake.

Hata hivyo, kauli ya Ntobi imeibua mjadala miongoni mwa wanachama wa CHADEMA na wachambuzi wa siasa kutokana na historia yake ya kumkosoa vikali Tundu Lissu, hususan katika kipindi cha kampeni za uchaguzi wa ndani ya chama.

Ntobi, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga, alijipatia umaarufu kwa matamshi yake ya moja kwa moja dhidi ya Lissu. Katika kipindi cha siku kadhaa kabla ya uchaguzi wa uongozi wa CHADEMA, Ntobi amewahi kumkosoa Lissu kwa kile alichokielezea kama “uropokaji” na kushindwa kuwa na busara katika maamuzi ya kisiasa.

Moja ya kauli zake zilizonukuliwa zaidi ni pale alipomtaja Lissu kama “mropokaji”, ‘mbea’ na kumshutumu kuwa hana uwezo wa kutunza siri za chama. Aidha, Ntobi alidai kuwa Lissu hakuwa mtu sahihi kuongoza CHADEMA kutokana na tabia zake, ambazo alizitaja kuwa za kuharibu mahusiano ya chama na wadau wake wa kitaifa na kimataifa.

Pia amewahi kumtuhumu Lissu kufadhili na kuunda kikosi kilichokuwa kinatumia jina la ” Sauti ya Wananchi” akishirikiana na watu maarufu mtandaoni na maafisa wa CCM, idara ya usalama wa taifa na Diaspora kwaajili ya kumfitini Mbowe

Aidha Ntobi amekuwa akimuhusisha na baadhi ya matendo yasiyofaa kimaadili kupitia maandikio yake akimuhusisha na “Mzungu” hasa pale Lissu anapokuwa safarini nje ya nchi kama ” Soon ataweka wazi faragha za mzungu wake” pamoja na “Si tuliwaambia jamaa yenu kakimbilia kwa mtasha wake? kiko wapi?”.

Kauli hizi, pamoja na nyingine nyingi, zilisababisha Kamati Tendaji ya CHADEMA Kanda ya Serengeti kufikia uamuzi wa kumvua Ntobi nafasi ya uenyekiti wa chama hicho mkoa wa Shinyanga mnamo Januari 8, 2025.

Licha ya historia hiyo, chapisho la hivi karibuni la Ntobi linaonesha mabadiliko makubwa ya msimamo. Katika ujumbe wake, Ntobi ameweka mbele mshikamano wa chama na umuhimu wa kuendeleza mapambano ya kidemokrasia. Pia, ameonesha nia ya kushirikiana na viongozi wapya wa CHADEMA ili kufanikisha malengo ya chama.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!