Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo amesema kuwa Jamhuri ya Indonesia itaendelea kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali.
Nyongo amebainisha hayo Julai 19, 2024 alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Pahala Mansury ambaye amefika nchini kwa ajili ya kuikaribisha Tanzania kwenye Kongamano la Biashara kati ya Indonesia na nchi za Afrika (Indonesia – Africa Forum).
“Ujumbe wa Jamhuri ya Indonesia, ukiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje umefika hapa kwa ajili ya kutualika kwenye Kongamano la Biashara litakalofanyika kuanzia Septemba 1-3, 2024 nchini Indonesia, sisi tumekubali kushiriki Kongamano hilo,” Amesema Nyongo.
Aidha, Nyongo amesema wamejadiliana masuala mbalimbali ikiwamo nchi hiyo ya Indonesia kuja nchini kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji wa Kilimo, uzalishaji wa nishati safi, pamoja na uwekezaji kwenye masuala mitandao mbalimbali, viwanda na miundombinu.
Nyongo amesema moja ya kampuni kutoka Indonesia ipo tayari kutekeleza mradi wa uzalishaji wa mbolea inayotakana na gesi hapa nchini utakaogharimu kiasi cha pesa Dola za Kimarekani bilioni 1.2.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Pahala Mansury amesema wameandaa Kongamano hilo la Biashara na nchi za Afrika ili kuimarisha ushirikiano kwenye masuala ya Uchumi hasa nchi ya Tanzania.
Mansury amesema Indonesia inaendelea kuwekeza nchini ikiwamo kwenye sekta muhimu za mafuta na gesi, uchakataji wa madini na masuala mengine ya uzalishaji wa chakula.
Kongamano hilo la Biashara litahusisha majadiliano kati ya mawaziri wa sekta mbalimbali, wafanyabiashara wa Indonesia na wafanyabiashara wa mataifa mbalimbali ya Afrika hasa Tanzania.