Kaimu Mkuu wa mkoa wa Arusha ambaye pia ni Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu ametangaza ufunguzi wa maonesho ya Nane nane kanda ya Kaskazini ambapo amesema maonesho hayo yataanza Agosti 01.2024 na kufunguliwa rasmi Agosti 03.2024
Akitoa taarifa hiyo kwa wanahabari leo, Ijumaa Julai 19.2024 jijini Arusha amesema maonesho hayo ya thelathini, maandalizi yake yameshaanza huku akiwaomba wananchi kujisajili na kulipia ada ya ushiriki wa maonesho hayo ambayo yamebeba kauli mbiu isemayeo ‘Chagua Viongozi bora wa Serkali za Mitaa kwa maendeleo endelevu ya Kilimo na Mifugo’
Aidha, Babu amesema kuwa serikali za mikoa hiyo ya kanda ya Kaskazini imewaomba wananchi kuendelea kujisajili huku ikiwaomba pia kuzingatia maelekezo yalivyoainishwa katika fomu iliyowekwa kwenye mtandao wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha ambapo amesema kuwa maonesho ya mwaka huu (2024) yatakuwa ya kipeke kuliko miaka mingine
Sambamba na hilo ametumia fursa hiyo kuzikaribisha taasisi za kitaifa na kimaitaifa huku akiwataka kuwasilisha maombi yao mapema ili kuondoa usumbufu katika siku za mwisho, hiyo ikienda sambamba na wafanyabiashara wadogo wadogo kutoka kanda hiyo kuchangamkia fursa hiyo
Pia, amewakaribisha wananchi wote wa kanda ya Kaskazini na wale wa mikoa mingine kufika mkoani Arusha katika maonesho hayo.