Wakili maarufu na mwanaharakati wa haki za binadamu, Onesmo Olengurumwa, ameandika ujumbe wa kipekee katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, akitoa wito wa upatanisho kati ya Freeman Mbowe na Tundu Lissu kabla ya uchaguzi wa nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho na Makamu wake, Tundu Lissu wanatarajiwa kupigiwa kura katika uchaguzi wa ndani wa CHADEMA ili kumpata kiongozi atakayeshika usukani na kukipeleka chombo kule ambako wanachama wanahitaji kufika.
Olengurumwa ameainisha umuhimu wa viongozi hao wawili kwa ustawi wa siasa za upinzani nchini Tanzania, akisema kila mmoja ana nafasi yake ya kipekee katika kujenga na kuimarisha mfumo wa vyama vingi nchini.
“Tunamhitaji sana Mhe. Lissu na siasa zake za mrengo mkali kupambana na wanaochezea demokrasia, lakini pia tunamhitaji Mhe. Mbowe na siasa zake za wastani na mazungumzo ya kimkakati,” amesema Olengurumwa.
Olengurumwa ameshauri kuwe na jitihada za kuwapatanisha Mbowe na Lissu kabla ya uchaguzi ili chama kiingie kwenye mchakato huo kikiwa na mshikamano.
“Napendekeza kuwe na upatanisho wa Mbowe na Lissu kabla ya uchaguzi. Faida ya upatanisho huu ni kwamba watakwenda kwenye uchaguzi wakiwa wamoja, lakini washindani wa kiti cha uenyekiti,” amesisitiza.
Wakili huyo pia amependekeza mabadiliko ya katiba ya CHADEMA baada ya uchaguzi, kwa lengo la kuweka ukomo wa madaraka, hatua ambayo amesema itasaidia kuimarisha mfumo wa chama hicho.
Olengurumwa amependekeza kuhusishwa kwa wazee mashuhuri na viongozi wa dini katika juhudi za kuleta suluhu. Miongoni mwa majina aliyopendekeza ni pamoja na Jaji Joseph Warioba, Joseph Butiku, na mwandishi maarufu Jenerali Ulimwengu. Akiweka msimamo wake, Olengurumwa amesema siasa za kupakana matope katika chaguzi za ndani za vyama ni hatari kwa mustakabali wa siasa za upinzani nchini.
“Binafsi siungi mkono siasa za kupakana matope, hasa kwenye chaguzi za ndani za vyama, kwa kuwa ni hatari sana kwa future ya upinzani nchini,” alisema.
Olengurumwa amewataka Mbowe na Lissu kufanya maamuzi yenye busara bila kusikiliza ushawishi wa wapambe na washabiki wao, akisisitiza kuwa bado anaamini katika mshikamano wao kwa ajili ya mustakabali wa siasa za upinzani nchini Tanzania.