Mahakama ya Rufaa ya Tanzania jijini Dar es Salaam leo, Jumatatu Julai 29.2024 imetoa uamuzi kuhusu rufaa iliyokuwa inapinga vifungu vya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ambavyo vinaruhusu watu kushtakiwa kwenye Mahakama ambazo hazina mamlaka ya kusikiliza kesi hizo
Akisoma uamuzi wa rufaa hiyo Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa Mheshimiwa Kingwele amesema jopo la Majaji watatu (3) wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam lilikosea pale Majaji hao wenyewe walipoamua kumpangia Jaji mmoja kati yao kusikiliza pingamizi lililopelekea kesi ya Onesmo Olengurumwa kutupiliwa mbali, jambo ambalo Mahakama ya Rufaa imeamua kwamba utaratibu sahihi ni kwamba endapo kuna pingamizi limewasilishwa Mahakamani Jaji Kiongozi au Jaji Mfawidhi ndiye anapaswa kupanga Jaji wa kusikiliza pingamizi hilo na sio Majaji wenyewe watatu (3) kuamua nani wa kusikiliza kati yao
Mahakama ya Rufaa kupitia uamuzi wake huo wa leo imeelekeza kesi hiyo irudi tena Mahakama Kuu kwa ajili ya kupangiwa Jaji wa kusikiliza pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa serikali mwaka 2019 kuwa kesi hiyo inafanana na kesi iliyowahi kuamuliwa miaka ya nyuma (kesi ya Galeba)
Kesi hiyo ilisikilizwa Julai 09.2024 mbele ya jopo la Majaji watatu (3) wa Mahakama ya Rufaa ambao ni Mheshimiwa Jaji Mlacha, Mheshimiwa Jaji Mwarija na Mheshimiwa Jaji Rumanyika
Ikumbukwe kuwa kesi hiyo ilifunguliwa na mtetezi wa Haki za Binadamu Wakili Onesmo Olengurumwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mwaka 2021 na ilisikilizwa Julai 09.2024 katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania, jijini Dar es Salaam mbele ya jopo la Majaji hao watatu (3).
Rufaa hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania masijala ya Dar es Salaam uliotolewa mwaka 2020 ambapo Mahakama Kuu ilitupilia mbali kesi hiyo kwa misingi ya kwamba aina ya maombi na kiini cha msingi katika maombi hayo, tayari ilikwisha amriwa katika mashauri ya awali (Res Judicata)
Kesi hiyo ilikuwa inapinga vifungu vya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai vinavyoruhusu washtakiwa kushtakiwa kwenye Mahakama za chini ambazo hazina mamlaka ya kusikiliza kesi hizo (Committal Proceedings)
Vifungu vilivyolalamikiwa ni namba 178, 243, 244, 245, 246, 247, 248, 249, 250, 256, 257, 258 na 259 vya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) kwa minajili ya kuwa vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Haki za Binadamu kwa mfano haki ya kusikilizwa kwa usawa, usawa mbele ya sheria nk, ambazo zipo katika Ibara ya 13(1)(2) na (6)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977
Hoja za Rufaa zilikuwa mbili ambazo ni:
(i) Mahakama Kuu ilikosea kutupilia mbali kesi hiyo kwa kigezo kuwa kiini na aina ya kesi hiyo ilikwisha amriwa katika kesi ya Galeba, kwa sababu kesi ya Galeba ilipinga vifungu viwili (2) tu, wakati kesi ya Olengurumwa inapinga vifungu 13 vya CPA
(ii) Kwamba jopo la Majaji wa Mahakama Kuu walikosea wao kama wao kumpangia Jaji mmoja kati yao ili kusikiliza pingamizi lililopelekea kesi hiyo kutupwa kinyume na utaratibu ambapo ilitakiwa Jaji Kiongozi ndiye apange Jaji mmoja kwa ajili ya kusikiliza pingamizi.