Latest Posts

OLENGURUMWA- AZAKI ZINATAKIWA KUJITEGEMEA KIFEDHA, ZISITAFUTE MISAADA NJE

Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa, amezitaka Asasi za Kiraia (AZAKI) nchini kuhakikisha zinajenga mifumo imara ya kifedha ili kuepuka utegemezi wa misaada ya nje.

Kupitia taarifa ya pamoja ya THRDC na East African Human Rights Institute ya tarehe 10 Februari 2025, Olengurumwa amesema ni wakati wa AZAKI kujifunza kutoka kwenye changamoto zilizotokea baada ya baadhi ya wahisani wa kimataifa, kama USAID, kupunguza au kusitisha ufadhili wao.

Kwa miaka mingi, AZAKI zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii, hususan kwenye sekta za afya, elimu, haki za binadamu, na maendeleo ya kijamii. Hata hivyo, utegemezi mkubwa wa fedha kutoka nje umesababisha miradi mingi kuyumba au kusimama pale misaada inapokatizwa.

Olengurumwa amesisitiza kuwa hali hii inapaswa kuwa chachu kwa AZAKI kuanza kujenga mbinu za kujitegemea kifedha ili kuhakikisha miradi yao inaendelea kwa ufanisi hata bila misaada ya wahisani wa nje.

Amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa sehemu kubwa ya misaada kutoka USAID imekuwa ikienda kwa mashirika ya kimataifa, huku mashirika ya ndani yakipata asilimia ndogo ya ufadhili. Hali hii imezua mjadala mpana kuhusu namna AZAKI za ndani zinavyoweza kujijenga kifedha ili kuepuka utegemezi wa wahisani wa nje.

Olengurumwa amependekeza AZAKI kushirikiana na sekta binafsi, kuanzisha miradi ya kibiashara, na kujenga mifumo ya michango ya wanachama kama njia mbadala za kujiongezea mapato. Ameeleza kuwa ni muhimu kwa AZAKI kuwa na mikakati thabiti ya kifedha ili kujiimarisha na kuendesha shughuli zao kwa uhuru na uendelevu.

Aidha, ametoa wito kwa serikali kuweka mazingira wezeshi kwa AZAKI ili ziweze kujitegemea na kuendelea kutoa huduma kwa jamii bila kutetereka. Kwa kufanya hivyo, AZAKI zitakuwa huru zaidi na miradi yao itaendelea kuhudumia wananchi hata katika mazingira yenye changamoto za ufadhili wa nje.

Mapema mwanzoni mwa mwaka huu mara baada ya kuapishwa na kuingia Ikulu, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kupitia mamlaka ya Rais (Executive Orders) kuzuia fedha zote za misaada zilizokuwa zinatolewa na serikali ya Marekani kupitia taasisi zake ikiwemo taasisi ya misaada ya Marekani (United States Agency for Development–US-AID).

Marekani imekuwa nchi kubwa duniani inayoongoza kutoa misaada kwa nchi zaidi ya 100 duniani kwa kutumia pesa za walipakodi wake. Katika mwaka wa fedha wa 2023, Tanzania ilipokea Dola milioni 630 (sawa na Shilingi za Kitanzania trilioni 1.61). Kiasi hiki kiliiweka Tanzania miongoni mwa nchi 20 zilizoongoza kwa kupokea misaada kutoka USAID, ikishika nafasi ya 18 duniani na ya 10 barani Afrika,

Misaada hiyo imekuwa ikitolewa moja kwa moja kwa serikali kupitia makubaliano ya pande mbili, kupitia mashirika ya Kimarekani na ya kimataifa yanayofanya kazi nchini na msaada mwingine huelekezwa kwa asasi za kiraia za Kitanzania (CSOs) zinazotekeleza miradi mbalimbali, na misaada mingine hupitia kampuni za biashara mbalimbali.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!