Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa amependekezwa kuwa miongoni mwa wagombea watatu bora wa nafasi ya Mwandishi na Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Watetezi wa Haki za Binadamu Duniani. Hatua hiyo inamfanya Olengurumwa kuwa mmoja wa wataalamu wa kwanza kutoka Tanzania kufikia hatua hiyo ya juu katika mfumo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa iliyotolewa Januari 26, 2026 na THRDC, imeelezwa kuwa kuteuliwa kwa Wakili Olengurumwa kumetokana na mapendekezo ya Kamati ya Ushauri ya Umoja wa Mataifa kwa Rais wa Baraza la Haki za Binadamu wakati wa Kikao cha 61 (HRC61).
Mchakato wa Kimataifa Mchakato huo ulikuwa wa ushindani mkubwa, ukihusisha wagombea 65 kutoka maeneo mbalimbali duniani waliokidhi vigezo. Kamati ya Ushauri imemchagua Olengurumwa kutokana na uzoefu wake wa zaidi ya miaka 10, uadilifu, na mchango wake mkubwa katika kulinda haki za binadamu nchini Tanzania, Afrika Mashariki, na barani Afrika kwa ujumla.
THRDC imebainisha kuwa utambuzi huu ni matunda ya uongozi wake thabiti akiwa Mwanzilishi na Mratibu wa Kitaifa wa kwanza wa mtandao huo. Chini ya uongozi wake, THRDC imekuwa sauti yenye ushawishi katika mageuzi ya sera na mifumo ya ulinzi kwa watetezi wa haki za binadamu katika ngazi za kitaifa na kimataifa.
“Amekuwa mstari wa mbele katika kujenga moja ya mifumo yenye uaminifu na ushawishi mkubwa zaidi kwa ajili ya ulinzi, uwezeshaji, na sauti ya pamoja ya watetezi wa haki za binadamu. Chini ya uongozi wake, THRDC imeweza kukua zaidi na kuwa mtandao unaoheshimika na wenye ushawishi mkubwa kitaifa, kikanda, na kimataifa, ukitoa mchango mkubwa katika mageuzi ya sera, mifumo ya ulinzi, utetezi, na mshikamano kwa watetezi wa haki za binadamu”, imeeleza sehemu ya taarifa ya THRDC.
Hatua hii imetajwa kuwa ni chanzo cha hamasa kwa watetezi chipukizi wa haki za binadamu Tanzania na Afrika, ikionesha kuwa utetezi wa ndani wenye misingi thabiti unaweza kutambulika katika ngazi za juu zaidi duniani.
Ingawa uteuzi wa mwisho unategemea uamuzi wa Rais wa Baraza la Haki za Binadamu, kufikia hatua ya tatu bora tayari ni ushindi wa kihistoria kwa sekta ya asasi za kiraia nchini.