Latest Posts

ONGEZEKO LA MATUKIO YA UTEKAJI TANZANIA LAITIA WASIWASI LHRC

Na Amani Hamisi Mjege.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu kuongezeka kwa matukio ya utekaji na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Tanzania, wakati kikizindua maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu kwa mwaka 2024.

Katika uzinduzi huo uliofanyika tarehe 17 Oktoba 2024, LHRC imesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vitendo vya utekaji, vitisho, na mauaji ya raia wasio na hatia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu nchini.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Usawa – Kupunguza Ukosefu wa Usawa na Kukuza Haki za Binadamu,” ikiwa na lengo la kuchochea juhudi za kimataifa za kupambana na ukosefu wa usawa na kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na kuheshimiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt. Anna Henga, amebainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la vitendo vya uvunjifu wa haki nchini, hususan vitendo vya utekaji ambavyo vinaathiri raia wa kawaida, ikiwa ni pamoja na watoto na wenza.

“Kwa nchi ya Tanzania, maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu kwa mwaka 2024 yanashuhudia kuongezeka kwa matukio ya kikatili yanayokiuka haki za binadamu nchini, ikiwemo vitendo vya kutishiwa, utekaji na mauaji ya watu wasio na hatia ikiwa ni pamoja na wenza na watoto”, amesema Dkt. Henga.

Kando na matukio ya utekaji, LHRC pia imeeleza wasiwasi kuhusu sheria kandamizi zinazominya uhuru wa vyombo vya habari na maudhui ya mitandaoni, hali inayozorotesha zaidi haki ya kupata taarifa na kujieleza. Kituo hicho kimehimiza serikali na vyombo vya usalama kuchukua hatua za haraka ili kurejesha hali ya ulinzi wa haki za binadamu nchini.

Katika kuadhimisha Siku ya Haki za Binadamu mwaka huu, LHRC imepanga matukio mbalimbali yanayolenga kuelimisha umma kuhusu haki za binadamu na usawa, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi, hususani wanawake, na kuandaa mashindano ya sanaa kwa wanafunzi wa shule za Dar es Salaam.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!