Mbunge wa Jimbo la Ilala na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, amesema wamefikia makubaliano ya kisheria zaidi ya asilimia 90 na kampuni ya Oryx Gas Tanzania kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa tanki kubwa la kisasa la gesi ambalo litagharimu zaidi ya Shilingi milioni 300 katika soko la Kimataifa la Samaki Feri jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Septemba 14, 2024, jijini Dar es Salaam, wakati wa kuutambulisha mradi huo, Mbunge Zungu alisema wafanyabiashara, hasa wale wanaokaanga samaki katika soko hilo, wamekuwa wakikumbana na hasara kubwa kutokana na matatizo ya matumizi ya mitungi ya gesi. Hali hiyo imesababisha asilimia 45 ya mitungi hiyo pekee kuwa na uwezo wa kufanya kazi, huku nyingine zikiganda na kuwa barafu.
“Kutokana na hasara hiyo, tumeona kuwa ni muhimu kuanzisha mradi wa tenki la gesi la jumla ambalo kila mtu atakuwa na luku yake na matumizi yake. Hii itasaidia kuboresha matumizi ya gesi kwa gharama nafuu,” alisema Zungu.

Aliongeza kuwa mradi huo unachangia katika jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kutunza mazingira, akieleza kwamba matumizi ya kuni na mkaa yanaharibu mazingira. “Tunamshukuru sana kampuni ya Oryx Gas kwa kushirikiana na halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ili kusaidia wafanyabiashara wa kukaanga samaki kupata nishati safi na salama kwa gharama inayowezekana,” alisema.
Zungu alifafanua kwamba mpaka sasa hatua za kisheria zimekamilika kwa asilimia 90 na kuwa jitihada hizi ni sehemu ya maelekezo ya Rais Dk. Samia kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli zao kibiashara kwa gharama za chini. “Viongozi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala walifanya jitihada kubwa kuhakikisha mchakato wa ujenzi wa tanki hilo unatekelezwa na walihakikisha kupatikana kwa eneo la mradi huu. Mradi huu unalenga maslahi mapana kwa wafanyabiashara, mazingira, na taifa kwa ujumla,” alisema Zungu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania, Ashelly Mbasha, alisema mradi huo ni mkubwa na utagharimu zaidi ya Shilingi milioni 300 hadi utakaporekebishwa, na wanatarajia kuanza mapema iwezekanavyo.
“Tunachokiomba Oryx ni ulinzi wa miundombinu mradi utakapoanza, kwani tunaweka miundombinu ya gharama kubwa kwa sababu gesi inahitaji usalama mkubwa. Tunaomba ulinzi wa hii miundombinu ili iweze kusaidia wafanyabiashara wote,” alisema Mbasha.
Mbasha alisisitiza kuwa Oryx Gas itaendelea kushirikiana na Serikali na kuwashukuru viongozi wa Manispaa ya Ilala kwa ubunifu huu.
“Tunampongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kampeni yake ya kuhakikisha hadi mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi. Tunaendelea kuwakaribisha wadau wote kutoka sekta binafsi, mashirika, na taasisi ili kuhakikisha ajenda ya Rais inafikiwa,” aliongeza.
Mbasha alisisitiza kuwa makubaliano ya awali yameshafikiwa na sasa wako katika hatua za mwisho za kuanza utekelezaji wa mradi. Alisema wanashukuru kwa hatua hiyo na wanahitaji ushirikiano wa wafanyabiashara wa soko hilo na wadau ili mradi ukamilike kwa wakati uliojiwekea.
Awali, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omar Kumbilamoto, alieleza kwamba Naibu Spika na Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Zungu, anafanya kazi kubwa kumsaidia Rais Samia, na yale yanayofanyika katika soko hilo yanatokana na maelekezo ya Rais ya kubadilisha matumizi ya kuni na mkaa na kuingia katika matumizi ya gesi.
“Niwaombe wafanyabiashara kupokea mabadiliko, ingawa yanachangamoto, lakini matumaini yangu ni kwamba watayakubali muda si mrefu. Nawashukuru Oryx kwa kuleta msaada wa zaidi ya Shilingi milioni 300,” alisema Kumbilamoto.

Kumbilamoto alimpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, kwa kusaini mkataba wa mradi wa tanki kubwa la gesi ya Oryx siku tatu zilizopita na kusisitiza kwamba kinachosubiriwa sasa ni kuanza utekelezaji, kwani vibali vyote vya kuruhusu mradi huo vimeshakamilika.
Aidha, Kumbilamoto aliwaomba wafanyabiashara kutoa ushirikiano kwa Oryx kwani mradi huo una lengo la kuboresha mji wa Dar es Salaam kwa kufuata kauli ya Rais Dk. Samia ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
“Sasa dunia inamtambua Rais kama Championi wa mazingira, na sisi tunawajibu kama wasaidizi wake kumsaidia. Mchakato wa kubadilisha matumizi ya gesi hauna kipaumbele kingine zaidi ya hiki, hivyo ni muhimu kutoa ushirikiano,” alisisitiza.