Latest Posts

PADRI KITIMA AJERUHIWA USIKU KURASINI, POLISI WAMSHIKILIA MTU MMOJA

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kuhusika katika shambulio dhidi ya Padri Charles Kitima, Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), aliyejeruhiwa kichwani na kitu butu akiwa katika eneo la maliwato ya kantini ya TEC, Kurasini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Mei 1, majira ya saa nne na robo, muda mfupi baada ya Padri Kitima kuhitimisha kikao cha viongozi wa dini kilichofanyika tangu saa tatu asubuhi hadi saa moja jioni.

“Baada ya kikao, Padri Kitima alielekea kwenye kantini ya baraza na kubaki hapo hadi saa nne na robo usiku, alipokwenda maliwatoni na ndipo alipojeruhiwa kichwani na watu wawili waliotumia kitu butu,” imeeleza taarifa ya polisi.

Padri Kitima alikimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan ambapo anaendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaelezwa kuwa inaendelea vizuri.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linamshikilia Rauli Mahabi @Haraja, mkazi wa Kurasini, kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo na linafanya uchunguzi wa kina wa chanzo cha tukio hili na kuwachukulia hatua kali na za haraka wote waliohusika.

Awali baadhi ya mashuhuda na waumini wa Kanisa hilo waliokuwepo kwenye mgahawa mmoja ndani ya Viunga vya TEC, Kurasini walieeleza Jambo TV kuwa Padri Kitima akiwa kwenye mazungumzo na baadhi ya watu, alinyanyuka na kuelekea msalani na ghafla kwa dakika chache walitokea watu waliomshambulia kwa sekunde chache na kisha kuondoka, na baadaye ndipo Padri Kitima alipoonekana akiomba msaada akiwa anavuja damu katika sehemu mbalimbali za mwili wake.

Mara baada ya shambulizi hilo, Padri Kitima amepatiwa matibabu ya awali kwenye kituo kidogo cha afya cha TEC kilichopo eneo hilo.

Padri Kitima kando ya utumishi wake na nafasi aliyonayo ndani ya Kanisa, amejipatia umaarufu mkubwa nchini Tanzania kwa miaka ya hivi karibuni kwa namna ambavyo amekuwa mkosoaji mkubwa wa mienendo isiyofaa kwenye jamii na akiwa mstari wa mbele katika kuhubiri utawala wa sheria na haki za binadamu pamoja na Demokrasia.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!