Latest Posts

PM MAJALIWA: TANZANIA INAFANYA MAPITIO YA SERA ZA FEDHA ILI KUDHIBITI MADENI

Na Amani Hamisi Mjege.
 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameainisha hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kushughulikia mzigo wa madeni ambao umekuwa changamoto kwa nchi zinazoendelea.
 
Akihojiwa na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, kando ya Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Majaliwa amezungumzia juhudi za Tanzania katika kuhakikisha madeni haya hayakwamishi maendeleo ya taifa.
 
Majaliwa amekiri kuwa nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo, zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni kutokana na mikopo kutoka kwa mataifa yaliyoendelea. Alibainisha kuwa, “Nchi kadhaa zimeshindwa kuendesha shughuli zao kutokana na fedha nyingi walizopata kwenda kulipa madeni,” huku akiongeza kuwa Tanzania nayo inakabiliwa na changamoto hiyo.
 
Katika kukabiliana na tatizo hilo, Waziri Mkuu amesema kuwa Tanzania imeanza kufanya mapitio ya sera zake za fedha ili kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo na mahitaji muhimu kama vile miundombinu, afya, elimu, kilimo, na maji vinaendelezwa bila kuzorota.
 
“Tunapata mapato ya ndani lakini bado hayatoshi kutoa huduma zote kwa wananchi wetu, hivyo tunahitaji kukopa.” Amesema Majaliwa.
 
Majaliwa amefafanua zaidi kwamba hatua ya serikali ni kudhibiti mapato ya ndani na kuongeza vyanzo vya mapato ili nchi iweze kulipa madeni na kubaki na fedha za kuendesha shughuli nyingine za maendeleo. Pia ameongeza kuwa serikali inaimarisha usimamizi wa mapato ya ndani na kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinatumika kwa malengo yaliyoainishwa, ikiwamo ulipaji wa madeni.
 
Waziri Mkuu ameendelea kutoa wito kwa mataifa yaliyoendelea kuzingatia utoaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa nchi zinazoendelea, kwani mahitaji ya maendeleo ni makubwa na nchi hizo haziwezi kuacha kukopa.
 
“Tunatoa wito kwa mataifa makubwa yanayotoa mikopo kuangalia viwango vya riba wanavyotoza ili nchi zinazoendelea ziweze kukopa, kuendesha miradi yao ya maendeleo, na kurejesha mikopo kwa urahisi,” amesema.
 
Majaliwa amehitimisha kwa kusisitiza kuwa mikopo yenye riba kubwa inazikandamiza nchi zinazoendelea, na kupelekea nchi hizo kushindwa kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!