Latest Posts

PM MWIGULU: MATAIFA MENGINE YANATUHUSUDU KWA NAMNA TUNAVYODHIBITI RUSHWA

Waziri Mkuu wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka Watanzania kujivunia mifumo ya nchi yao katika kusimamia rasilimali na kusema kuwa Tanzania bado ni “mwalimu” kwa mataifa mengi ya Afrika katika suala la utawala bora.

Akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) leo mkoani Morogoro kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Mwigulu amevipongeza vyombo vya udhibiti, hususan TAKUKURU, kwa kazi kubwa inayofanya nchi iaminike hata nje ya mipaka.

Waziri Mkuu amewajibu watu na mataifa yanayoikosoa Tanzania mitandaoni, akieleza kuwa wengi wao wanahangaika na Tanzania kwa sababu wameshindwa kufikia kiwango cha udhibiti uliopo hapa nchini. Amesema kuwa katika nchi nyingine, rushwa ndogo tu ya kiwango cha Diwani inaweza kuangusha serikali, lakini Tanzania imejenga mifumo imara inayozuia mianya hiyo.

Waziri Mkuu amekwenda mbali zaidi kwa kutoa mfano wa namna fedha za umma zinavyosimamiwa, akibainisha kuwa tofauti na nchi nyingine ambapo Mbunge anaweza kupokea fedha za maendeleo kwenye akaunti yake binafsi, Tanzania ina taratibu kali zinazozuia mbunge hata kugusa fedha za Mfuko wa Jimbo. Alisisitiza kuwa nidhamu hiyo ya matumizi ndiyo inayofanya rasilimali za nchi ziwafikie wananchi na kuleta maendeleo ya kweli.

Aidha PM Mwigulu amewasilisha ujumbe mzito kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa mkuu huyo wa nchi hapendi na wala havumilii vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, na uzembe kazini.

Akizungumza na viongozi hao wa TAKUKURU, Waziri Mkuu amebainisha kuwa dhamira ya Rais Samia ya kulinda utu wa mwananchi na kuhakikisha maendeleo ya taifa inategemea sana uadilifu na uwajibikaji wa taasisi za udhibiti. Ameeleza kuwa Rais amekuwa akifanya juhudi za makusudi kuziimarisha taasisi hizo kwa kuziongezea rasilimali watu, bajeti, miundombinu, na hata kufanya marekebisho ya kisheria ili kuzipa “meno” ya kutosha kutekeleza majukumu yao.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa kupitia kazi nzuri inayofanywa na TAKUKURU, rasilimali za nchi zitatumika ipasavyo kwa ajili ya kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli. Amewataka viongozi hao kupokea salamu za Rais na kuendelea kupambana na vitendo vyote vinavyoharibu misingi ya utawala bora, huku wakijua kuwa wana uungaji mkono wa asilimia 100 kutoka ngazi ya juu ya uongozi wa nchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!