Jeshi la Polisi Tanzania limethibitisha kuwa linafanyia kazi taarifa zinazodai kuwa aliyewahi kuwa Mbunge na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, ametekwa, kufuatia madai yaliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa leo, Oktoba 6, 2025, na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu Dodoma, DCP David Misime imesema kuwa tayari uchunguzi umeanza ili kubaini ukweli wa taarifa hizo, huku likisisitiza kuwa bado linaendelea kumsubiri Polepole aripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
“Jeshi la Polisi limeona taarifa zinazosambazwa kwenye Mitandao ya Kijamii na ndugu zake kuwa ametekwa, tayari tumeanza kufanyia kazi taarifa husika ili kupata ukweli wake”, imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, Polepole alitumiwa barua ya wito kisheria akitakiwa kufika mbele ya DCI ili kutoa maelezo kuhusu tuhuma mbalimbali alizozitoa kupitia mitandao ya kijamii, lakini hadi sasa hajatekeleza agizo hilo.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa wito huo ulitolewa kwa mujibu wa sheria za nchi, na linatarajia Polepole ataripoti kwa hiari yake ili kusaidia katika uchunguzi unaoendelea.
Taarifa hiyo, iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Dodoma, imehitimisha kwa kusisitiza kuwa Jeshi linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba na sheria, likizingatia weledi na haki katika kila hatua ya ufuatiliaji wa tuhuma hizo.