Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, likiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, SACP Allan Kubumbi, limetembelea na kutoa msaada kwa watoto wenye uhitaji katika vituo vya watoto yatima vya Faraja kilichopo eneo la Mgongo pamoja na Kituo cha Dar-Fatma na Dar-Bilaal kilichopo Ilala ndani ya Manispaa ya Iringa.
Msaada huo ni sehemu ya jitihada za Jeshi la Polisi katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, pamoja na kuendelea kujenga ukaribu na jamii na kuimarisha ushirikiano katika kulinda haki na ustawi wa mtoto.

Katika ziara hiyo, mahitaji mbalimbali yalitolewa yakiwemo sukari, sabuni, unga wa ngano na sembe, mchele, maharagwe, taulo za kike pamoja na vifaa vya shule na mahitaji mengine muhimu.
Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha na walezi pamoja na watoto, wakieleza shukrani zao kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kwa kuonyesha upendo na mshikamano kwa jamii.