Latest Posts

POLISI MARA WASHIKILIA WANACHAMA 27 WA BAWACHA; WADAI WALIFANYA UCHOCHEZI NA KUZUIA BARABARA.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mkoani Mara yamegubikwa na taharuki baada ya Jeshi la Polisi kutawanya msafara wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) kwa mabomu ya machozi, huku likiwashikilia watu 27 kwa tuhuma za kufanya vurugu na uchochezi.

Tukio hilo limetokea leo, Machi 8, 2026, katika Barabara ya Nyerere mjini Musoma, mara baada ya wanachama wa BAWACHA kumaliza ibada ya misa katika Kanisa Katoliki.

 

Kauli ya BAWACHA: “Polisi Wametupiga Mabomu Mchana Kweupe”

Mwakilishi wa BAWACHA Taifa, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti Sharifa Suleiman, amelaani vikali kitendo cha polisi kutumia nguvu kubwa kuzuia maadhimisho yao. Amesema kuwa lengo la mkutano wao lilikuwa ni kujadili changamoto zinazowakabili wanawake na kujenga mikakati ya kimaendeleo.

Vilevile, BAWACHA wamelalamikia kitendo cha polisi kuwanyang’anya sare za chama na kuwakamata viongozi wakuu, akiwemo Katibu Mkuu wa baraza hilo.

“Sare za BAWACHA sio madawa ya kulevya. Inakuwaje Jeshi la Polisi wanawanyang’anya wanawake nguo zao? Walitarajia waende uchi? Tunalitaka jeshi kuwaachia viongozi wetu mara moja na kurejesha vifaa vyetu,” alisema mtoa taarifa wa BAWACHA.

 

Kauli ya Polisi: “Walikuwa Tayari Kufa, Tulizuia Uchochezi”

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, SACP Pius Lutumo, amethibitisha kuwashikilia watu 27 na kueleza kuwa hatua hiyo ilifuatia ukaidi wa BAWACHA dhidi ya katazo la kisheria lililotolewa Machi 1, 2026. RPC Lutumo amedai kuwa maandalizi ya BAWACHA yaliambatana na kauli za uchochezi kama “hawaogopi polisi” na “wako tayari kufa”.

Kamanda Lutumo amefafanua kuwa polisi hawakuzuia ibada, bali walidhibiti vurugu zilizoanza baada ya wanawake hao kuungana na vikundi vya vijana barabarani na kuanza kuzuia shughuli za kijamii na kiuchumi katika barabara kuu ya Musoma-Bunda.

“Jeshi la Polisi lilifanikiwa kudhibiti wafanya vurugu hao na kuwatawanya ili barabara zifunguke. Tunatambua haki ya kuabudu, lakini hatutaruhusu uvunjifu wa sheria kwa kisingizio cha maadhimisho,” alisisitiza SACP Lutumo.

 

Mvutano wa Kidemokrasia

Wakati BAWACHA wakitafsiri kitendo hicho kama unyanyasaji wa kijinsia na jitihada za kuziba sauti za wanawake kuelekea uchaguzi, Jeshi la Polisi linashikilia msimamo kuwa usalama wa mkoa ni kipaumbele na kwamba walichukua hatua kuzuia taharuki zaidi kwa wananchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!