Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linawashikilia askari wawili wa Jeshi la Magereza, Sijali William Hence na Ilinus Mushumbusi, kwa tuhuma za kuhusika katika kifo cha Emmanuel Lucas (18), mkazi wa Kijiji cha Kisangura, wilayani Serengeti.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, tukio hilo lilitokea Machi 31, 2025, majira ya saa 4:00 asubuhi ndani ya kambi ya mradi wa ufugaji katika gereza la Tabora B. Askari hao watatu waliokuwa zamu walikamata ng’ombe 98, mbuzi 5, na kondoo 6 waliokuwa wameingizwa ndani ya eneo hilo kinyume cha utaratibu.
Hata hivyo, wakati mifugo hiyo ikipelekwa kuhifadhiwa ndani ya kambi, kundi la vijana wapatao 20, wakiwa na silaha za jadi kama mapanga na mishale, walivamia eneo hilo na kuwashambulia askari hao wakidai waachie mifugo yao.
“Katika jitihada za kujiokoa kutoka kwenye kundi hilo la vijana, askari hao walifyatua risasi kadhaa hewani kwa lengo la kuwatawanya. Moja ya risasi hizo ilimjeruhi Emmanuel Lucas, ambaye alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa hospitalini,” imeeleza taarifa ya Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini mazingira halisi ya tukio hilo na hatua zaidi zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Polisi Mkoa wa Mara limewataka wananchi kuzingatia mipaka ya malisho ya mifugo yao ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.