Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limemkamata Paulo Shija (19), mkazi wa Ndala, Shinyanga, kwa tuhuma za kumjeruhi mke wake wa zamani, Ester Mataranga (25), kwa kutoboa macho yake yote mawili katika tukio la kikatili lililotokea tarehe 13 Agosti 2024.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth S. Magomi, Polisi walipokea taarifa za kujeruhiwa kwa Ester Mataranga na walichukua hatua za haraka kufika eneo la tukio, ambapo walimkuta majeruhi huyo akiwa katika hali mbaya.
“Baada ya kupokea taarifa hizo, Jeshi la Polisi lilichukua hatua za haraka kwa kufika eneo la tukio na kumchukua majeruhi huyo na kumpeleka katika Hospitali ya Kolandoto iliyopo Halmashauri ya Kishapu kwa ajili ya kupatiwa matibabu,” alisema Kamanda Magomi.
Kamanda Magomi alieleza kuwa baada ya tukio hilo, Polisi walianzisha msako wa kumtafuta Paulo Shija, kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo hayo.
“Jeshi la Polisi lilianza msako wa kumtafuta mtuhumiwa huyo kwa kushirikiana na wananchi na hatimaye, mnamo tarehe 17 Septemba 2024, Paulo Shija alikamatwa katika maeneo ya Masekelo, Manispaa ya Shinyanga,” alifafanua Kamanda huyo.
Mtuhumiwa huyo alipelekwa kituo cha Polisi kwa taratibu zaidi za upelelezi, na mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi, anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limekemea vikali vitendo vya kujichukulia sheria mikononi, likisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kufuata taratibu za kisheria.