Katibu wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo- CHADEMA (BAVICHA) Mkoa wa Mwanza, Amani Manengelo anadaiwa kutekwa na watu wanaodaiwa kuwa ni Maafisa wa Jeshi la Polisi.
Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu siku ya Jumatatu Februari 17, 2025 Katibu wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Zakaria Obad amedai Manengelo alitekwa Ijumaa Februari 14, 2025 akiwa wilayani Misungwi mara baada ya kupigiwa simu na watekaji kupitia simu ya rafiki yake wa kike (jina lake limehifadhiwa).
“Februari 14, 2025 alipigiwa simu na watu waliojitambulisha, ilikuwa kama mbinu yeye ana rafiki yake pale Misungwi anayejishughulisha na ususi wa kusuka wanawake wenzake. Siku hiyo akawa amepigiwa simu kwamba njoo hapa ninakungoja, alivyofika akakutana na watu fulani ambao hao watu kwa mujibu wa maelezo ya huyo dada walimpigia simu wakidai wanataka kusuka aina fulani ya msuko na wakakubaliana bei na kwa sababu walimkuta dada huyo anasuka wateja wengi wakabaki wanasubiri wakiwa akina dada wawili”, ameeleza Obad.
Obad amesema baada ya kusubiri kwa muda mrefu baadaye dada wale wakasema hawataki kusuka isipokuwa tu walikuwa na shida na mtu mmoja aitwaye Amani Manengelo, na kisha wakamuweka rafiki huyo wa kike chini ya ulinzi na kumfunga pingu wakisema wanataka kumpigia kupitia simu yake

“Baadae wakampigia Manengelo na kwa vile alipigiwa na mtu anayemfahamu akaenda, kwahiyo amefika pale akawakuta wale watu wakajitambulisha kuwa wanamtafuta na tayari walikuwa wamejitambulisha kwa huyo dada kwamba kuna fedha fulani ilitumwa kwa rafiki yake Manengelo sasa hatumpati kwahiyo tunataka atusindikize atusaidie tumpate aliko”, ameeleza.
Obad amedai baada ya Manengelo kufika eneo la tukio aliwekwa chini ya ulinzi ndipo wanaume wawili waliovalia kiaskari wakaongezeka na kumkamata kisha kuondoka naye wakidai anaenda kulisaidia Jeshi la Polisi kufanikisha kumkamata rafiki yake Manengelo aliyetumiwa fedha kisha kutokomea kusikojulikana, na simu zake hazipatikani tena tangu siku hiyo na wala hajaonekana kokote kule licha ya jitihada za kutafutwa.
“Lakini kingine ni kwamba yule mdada ambaye walikuwa wanatumia simu yake, baada ya kumkamata na kukamilisha misheni yao walichukua simu ya yule dada wakafuta namba zao,” amesema.
Kutokana na tukio hilo Obad amedai chama hicho kinatoa saa mbili kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha kiongozi huyo anaachiwa au kupatikana.
“Sisi tunaamini Jeshi la Polisi linajua huyu kijana yuko wapi ndiyo maana tumetoa muda wa saa 12 tumpate, tofauti na hivyo basi wajiandae kutufanyia chochote ambacho wanaweza kutufanya,” amesema Obad.
Jambo TV tumemtafuta kwa njia ya simu binafsi Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Audax Majaliwa ambaye hata hivyo hakupatikana kwenye simu. Hii ilikuwa ni baada ya juhudi kadhaa za kumtafuta kupitia simu ya ofisi ambayo ilikuwa ikiita pasina kupokelewa na baadaye tulipoipigia kwa mara nyingine haikupatikana kabisa. Hata hivyo juhudi za kuendelea kumtafuta Kaimu Kamanda huyo bado zinaendelea.