Latest Posts

POLISI WAJIBU MADAI YA CHADEMA: “TULIMKAMATA HECHE NA MNYIKA TU, HAKUNA ALIYEPIGWA”

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, Jumatatu, Aprili 28, 2025, amekanusha madai kuwa Jeshi la Polisi liliwapiga au kuwatesa wanachama wa Chadema waliokamatwa hivi karibuni, akibainisha kuwa walikamatwa viongozi wawili pekee wa chama hicho, ambao ni Makamu Mwenyekiti John Heche na Katibu Mkuu John Mnyika.

Akizungumza na chombo cha habari cha Jamii Forums, Muliro amesema, “Sisi tuliwakamata Heche na Mnyika, waliuzeni kama wana majeraha. Hao wengine tuwakamate tuwapeleke wapi? Waulizeni walikamatwa wapi?” amehoji, akisisitiza kuwa si kila aliyepata majeraha siku hiyo alijeruhiwa na Polisi.

Akizungumzia hali ya usalama katika viunga vya Mahakama ya Kisutu wakati wa kutajwa kwa kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, Muliro ameeleza kuwa wanachama wa Chadema walilazimika kuondolewa kutokana na kauli zao zilizodaiwa kuhatarisha usalama wa mahakama na shughuli nyingine.

“Sisi tuliweka mazingira mazuri kwa mahakama kufanya kazi. Kwani hao Chadema peke yao ndiyo wenye kesi? Pale Kisutu kuna mahakimu wangapi? Kama mahakimu wapo 20, kesi moja ya Lissu ndiyo isimamishe kesi nyingine 19?” amehoji Muliro, akieleza kuwa baadhi ya wanachama walitoa vitisho kuwa, endapo Lissu hatuachiwa, wangetoa hatua ambazo hazikufafanuliwa.

Katika hatua nyingine, Kamanda Muliro amezungumzia uamuzi wa Polisi kuzuia mkutano wa hadhara wa John Heche uliopangwa kufanyika Aprili 22, 2025, katika eneo la Kariakoo. Ameeleza kuwa utoaji wa taarifa ya mkutano mapema hauondoi mamlaka ya Polisi kuuzuia kama kuna viashiria vya hatari.

“Hatubishani na CCM, wakishauriwa jambo hukubali na hawapigi kelele, tuna ushahidi wa hilo,” ameongeza.

Kuhusu iwapo Jeshi la Polisi litaendelea kuzuia watu kuhudhuria vikao vya kesi za viongozi wa Chadema, Muliro amesema Polisi watachukua hatua dhidi ya mtu yeyote mwenye nia ya kufanya uovu kabla uhalifu haujatokea.

Hata hivyo, Aprili 25, 2025, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanachama 21 wa chama hicho walikamatwa na wengine kuteswa na kupigwa kabla ya kutupwa katika mapori maeneo mbalimbali ndani na nje ya Dar es Salaam, madai ambayo Polisi wameyakanusha.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!