Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limetoa ufafanuzi kuhusu video inayosambaa mitandaoni ikimuonesha raia wa kigeni, Silvia Vlaskamp, akidai kunyanyaswa, kufungiwa ndani ya nyumba, na kuibiwa mali zake na askari wa kampuni binafsi ya ulinzi.
Polisi wamesema tukio hilo lilitokea baada ya utekelezaji wa amri halali ya Mahakama ya kufilisi kampuni ya VASSO AGRO VENTURES, inayomilikiwa na Silvia pamoja na mumewe Alphonsius Nijenhius.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa Aprili 21, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, mume wa Silvia, Alphonsius, aliripoti Polisi Oktoba 25, 2024 kuwa alivamiwa na kuibiwa mali zenye thamani ya dola za Marekani 144,145, fedha taslimu Shilingi 120,000, na dola 9,900 pamoja na mifugo kuuawa na watu wanaodaiwa kuongozwa na Wakili Kester Paul Lyaruu.
Hata hivyo, Polisi walibainisha kuwa Wakili huyo alikuwa amepewa mamlaka na Mahakama Kuu Kanda ya Moshi kuwa mfilisi wa kampuni ya VASSO AGRO VENTURES L.T.D, baada ya Adrianus Johannis – mwekezaji kutoka Uholanzi na mmiliki wa kampuni ya MAPATO BV – kufungua shauri la madai No: 03/2023 akidai kampuni hiyo imeshindwa kurejesha mkopo wa Euro 1,200,000 waliokopeshwa mwaka 2020.
“Ukweli wa tukio hilo ni kuwa, mfilisi wa kampuni hiyo aliyeteuliwa na Mahakama, Wakili Kester Paul Lyaruu, aliambatana na askari wa kampuni binafsi ya ulinzi ya MX5 Security, pamoja na Mtendaji wa Kijiji cha Dakau, na kufika katika nyumba ya kampuni hiyo kwa lengo la kutekeleza agizo la Mahakama la kufunga na kufilisi kampuni,” amesema Kamanda Maigwa.
Kamanda Maigwa amesema Jeshi la Polisi limewachunguza watu 15 waliokuwa katika tukio hilo wakiwemo askari wa kampuni ya ulinzi ya MX5 na Meneja wao. “Jeshi la Polisi limehoji mlalamikaji pamoja na mashahidi wengine kuhusu tuhuma hizo kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria”.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Polisi, Silvia na mumewe walishuhudia wenyewe mali zao zikihamishwa, na wao ndio waliotafuta usafiri wa kuhamishia mali hizo mkoani Arusha kwa mtoto wao.
Kwa upande wake, Silvia Vlaskamp alizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma na kueleza kwa uchungu kuwa tukio hilo lilikuwa la “uvamizi haramu na wa kikatili”. Alidai kuwa Oktoba 24, 2024, alikumbana na askari waliomlazimisha kutoka ndani ya gari lake, kumshika kwa nguvu na kumdhulumu mali zake huku wakimnyang’anya simu aliyokuwa akiitumia kurekodi tukio hilo.
Silvia pia alieleza kuwa alifungiwa ndani kwa saa kadhaa na kwamba mumewe alijaribu kutoa taarifa Polisi Moshi lakini hakusaidiwa. Alidai kuwa baadaye waliovaa kiraia na askari walivunja mlango na kuanza kuchukua mali mbalimbali ikiwa ni pamoja na pesa taslimu, vito vya thamani, vifaa vya kielektroniki na hata nguo binafsi.
Amesema licha ya kufungua jalada la kesi lenye kumbukumbu namba MOS/RB/8476/024, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa miezi sita tangu tukio litokee. Ameiomba Serikali kuingilia kati na kuwalinda wawekezaji dhidi ya vitendo vya unyanyasaji, uporaji na ukatili.