Wakazi wa Kata ya Nyawilimilwa, Halmashauri ya Wilaya ya Geita, wameiomba serikali kupitia Jeshi la Polisi kuongeza doria katika eneo la pori linalotoka Bugulula kuelekea mjini Geita, wakieleza kuwa limegeuka kuwa kitovu cha matukio ya uhalifu ikiwemo utekaji wa watu na uporaji wa pikipiki.
Wakizungumza wakati wa mafunzo ya usalama kwa jamii yaliyoandaliwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML), wananchi wamesema licha ya kuwepo kwa juhudi mbalimbali, bado eneo hilo limeendelea kuwa hatarishi kwa maisha ya wakazi na hasa waendesha bodaboda.
Lucas Juma, mmoja wa wakazi wa Nyawilimilwa, amesema matukio ya mauaji na uporaji katika pori hilo yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara, hali inayowatisha wengi kushindwa kufanya shughuli zao kwa uhuru.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Elisante Ulomi ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Jamii, amesema tayari suala hilo lipo katika kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na hatua zinaendelea kuchukuliwa. Pia aliwataka wahalifu kuacha mara moja vitendo hivyo kwani vyombo vya dola vinaendelea kuwafuatilia kwa ukaribu.
Mgodi wa GGML umeahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa elimu ya usalama kwa wananchi kupitia kampeni ya Community Policing Outreach, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano baina ya jamii na vyombo vya dola katika kupambana na uhalifu.