Latest Posts

PPRA NA FDH WAWAPA MAFUNZO WENYE ULEMAVU DODOMA

Zaidi ya watu wenye ulemavu 200 wamepatiwa mafunzo kuhusu sheria za manunuzi ya umma, fursa zilizopo kwa makundi maalum, na matumizi ya Mfumo wa Nest wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA).

Mafunzo haya yamelenga kuwawezesha kunufaika na asilimia 30 ya bajeti ya serikali zinazotengwa kwa makundi maalum, ikiwemo asilimia 10 kwa wenye ulemavu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, akiwakilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Watu Wenye Ulemavu, Rashid Maftaha, ameeleza kuwa serikali imeimarisha juhudi za kuwezesha makundi maalum kupitia PPRA. Lengo ni kuwawezesha kushiriki katika zabuni za manunuzi ya umma, na kupatiwa ajira ili kuboresha hali zao za kiuchumi.

Kikwete amesema sheria za manunuzi zinatoa nafasi kwa watu wenye ulemavu kupitia mpango wa asilimia 30 wa bajeti ya umma kwa makundi maalum. Aidha, asilimia 2 ya mapato ya halmashauri hutengwa kwa ajili ya kundi hili kupitia mikopo, ili kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, CPA Salmini Malole, amebainisha kuwa vikundi maalum, ikiwemo vya watu wenye ulemavu, vimepata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.8 kwa mwaka huu wa fedha. Amehimiza watu wenye ulemavu kuchangamkia nafasi zilizopo kwenye Mfumo wa NeST ili kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika zabuni za umma.

Naye Mkurugenzi wa Foundation for Disabilities (FDH), Michael Salali, amesema mafunzo hayo yamehusisha makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu, wakiwemo wenye ualbino, wasioona, na walemavu wa viungo. Ameshukuru PPRA kwa kipaumbele walichotoa kwa kundi hili na kuwataka washiriki kutumia maarifa waliyopewa kujiajiri na kuondokana na umasikini.

Afisa Mahusiano wa FDH, Furahini Chemakaa, ametaja changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu, kama ukosefu wa uelewa wa lugha ya alama kwa baadhi ya wakuu wa taasisi za umma na binafsi, pamoja na utekelezaji hafifu wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya 2010 inayotaka waajiri kutenga asilimia 3 ya nafasi za ajira kwa kundi hili.

Mwenyekiti wa Bodi ya FDH, Dk. Henry Humba, ameishukuru serikali kwa juhudi zake za kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi kupitia sera na sheria mbalimbali. Amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuweka mazingira mazuri kwa kundi hili kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Mafunzo haya yanatarajiwa kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu kwa kuwapa fursa za kiuchumi, ajira, na ushiriki mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!