Latest Posts

PROF. KITILA: MASHIRIKA YA SERIKALI YAWE YA UMMA KWA WANANCHI KUMILIKI HISA

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa mageuzi ya kidijiti kama sehemu ya mkakati wa kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku ikiweka malengo madhubuti ya kuhakikisha huduma za serikali zinapatikana kwa njia ya mtandao ili kupunguza msongamano na mwingiliano wa moja kwa moja wa watu.

Akizungumza Jumatano Machi 26, 2025, wakati wa kufungua Mkutano wa Wakurugenzi wa Bodi za Kampuni ambazo Serikali ina Umiliki wa Hisa Chache, unaofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere wilayani Kibaha, mkoani Pwani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema:

“Katika Dira ya Maendeleo 2050, tumesisitiza umuhimu wa mageuzi ya kidijiti. Tumekubaliana kuwa lazima tufanye mabadiliko haya, na hata tunapanga malengo maalum kuhusu kiwango cha huduma za serikali kinachopaswa kupatikana mtandaoni ili kupunguza mwingiliano wa moja kwa moja.”

Profesa Mkumbo ameendelea kueleza kuwa serikali imejipanga kuimarisha mifumo ya utawala katika bodi za kampuni zake kwa kuhakikisha kuwa kuna uwajibikaji, uwazi, na uongozi wa maadili huku akitoa wito kwa kampuni ambazo bado hazijaanza kutoa gawio kwa serikali zianze kufanya hivyo kwa sababu nazo ni taasisi za kibiashara.

“Pia tunatarajia kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ili kuongeza tija katika uchumi wa taifa. Serikali na sekta binafsi lazima tushirikiane kwa karibu zaidi ili kufanikisha malengo yetu.”, ameeleza Prof. Kitila.

Waziri Mkumbo amesisitiza umuhimu wa kampuni hizo kuoanisha mikakati yao ya biashara na vipaumbele vya kitaifa vya kiuchumi.

“Nyinyi mnaofanya kazi kwenye kampuni hizo, tunaendelea kuwasihi kuhakikisha kuwa mikakati yenu ya biashara inaendana na mwelekeo wa kiuchumi wa taifa. Kila mmoja wetu anachangia katika maendeleo ya uchumi wa taifa, hivyo ni muhimu mipango, dira, na dhamira zenu za kampuni ziwe sambamba na mkakati wa kitaifa wa maendeleo.”, ameeleza.

Aidha, Waziri Mkumbo ameendelea kusisitiza wito wake wa kubadilisha mashirika ya serikali kuwa mashirika ya umma kwa kuhakikisha yanauzwa kwa umma kupitia masoko ya hisa.

“Mwaka jana nilitoa wito kuhakikisha kuwa mashirika ya kibiashara ya serikali yanageuka kuwa mashirika ya umma. Kwa sasa tunaviita mashirika ya umma, lakini kiukweli ni mashirika ya serikali. Ili shirika liwe la umma, wananchi wanapaswa kuwa na hisa ndani yake, jambo ambalo linaweza kufanyika tu kwa kuyaorodhesha kwenye soko la hisa. Wananchi wa kawaida wawe na nafasi ya kununua hisa na kuyamiliki moja kwa moja.”

Waziri amdhitimisha hotuba yake kwa kuwahimiza washiriki wa mkutano huo kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mazingira ya biashara nchini ili kukuza uchumi zaidi.

Mkutano huo, wenye kaulimbiu “Matumizi ya Teknolojia Kuboresha Utendaji”, umelenga kuangazia umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuongeza ufanisi wa mashirika yenye umiliki wa serikali wa hisa chache.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!