Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amesema wananchi wengi wa Tanzania wamependekeza serikali kushughulikia zaidi uchumi na ustawi wa jamii kwa kuongeza nafasi za ajira na uwekezaji kwenye huduma bora za kijamii.
Prof.Kitila ametoa kauli hiyo Julai 20, 2024 Jijini Mwanza, wakati wa uzinduzi wa Kongamano la Kwanza la Kikanda Kuhusu Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 linalofanyika ukumbi wa Kwatunza uliopo wilayani Ilemela mkoani Mwanza, na kusisitiza kuwa zaidi ya asilimia 81 ya waliotoa maoni yao kufikia sasa kwenye kuandaa dira hiyo ya maendeleo ni vijana kutoka maeneo mbalimbali.
Waziri Kitila Mkumbo ametaja vipaumbele vingine vilivyotajwa na wananchi waliotoa maoni yao ni uimarishaji wa sekta ya kilimo, viwanda, utalii na miundombinu mingine ya kijamii, akisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kutoa maoni yao kwa njia mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maelekeo ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.
Aidha Waziri Kitila amemwambia mgeni rasmi Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko kuwa asilimia 69 ya wananchi wanasema nchi ipo kwenye muelekeo sahihi huku zaidi ya asilimia 76 wakisema miaka 25 ijayo nchi itakuwa kwenye eneo zuri zaidi kutokana na kasi ya utekelezaji wa mipango mbalimbali.
Akizungumzia utekelezaji wa dira iliyopita, Waziri Kitila ametoa mfano wa ujenzi wa miundombinu akisema kuwa mwaka 1999 Tanzania ilikuwa na mtandao wa barabara wa kilomita 85,000 pekee na kufikia 2022 serikali imetekeleza mpango wake na kuwa na mtandao wa barabara wa kilomita 181,190 sawa na ongezeko la asilimia 181.