Wahitimu wa fani ya utabibu wa kinywa na meno pamoja na wauguzi kutoka Taasisi ya mafunzo ya afya na sayansi shirikishi Kibosho wameshauriwa kuongeza elimu yao na kuzingatia mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Ushauri huo umetolewa Julai 19.2024 katika mahafali ya 22 ya chuo hicho na Mgeni rasmi Prof.Patrick Ndakidemi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini ambapo amesema kuwa wahitimu katika taasisi hiyo wamekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya afya nchini.
“Ikiwezekana uongozi wa taasisi upandishe hadhi taasisi hii ili kuanza kutoa shahada za uuguzi kwani kada hiyo bado inahitaji wasomi wengi kutokana na kuwa wachache ikiwa miundombinu ya taasisi hiyo itaongezwa pamoja na wakufunzi” alishauri
Awali akisoma risala ya wahitimu wa chuo hicho Arimu Muninga amesema kuwa licha ya uwepo wa mafanikio,bado zipo changamoto zinazo kabili taasisi hiyo ikiwemo uhaba wa madarasa,ukosefu wa chanzo mbadala wa umeme,vifaa vya kufundishia ikiwemo kompyuta na uhaba wa viti katika Bwalo la kulia chakula na kuomba utatuzi wake.
Naye Mhisani wa taasisi hiyo ambaye ni Mwenyekiti wa soko la Kariakoo Jijini Dar es salaam na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro Martin Massawe ameahidi kusaidia taasisi hiyo vifaa vya Tehama vinavyo hitajika ili wanafunzi waondokane na changamoto ya ukosefu wa vifaa hivyo.
“Naomba niwashauri watanzania kukumbuka nyumbani kwani nyumbani ni nyumbani ni vema kusaidia tunapo toka ikiwa huko tulipo tunafanya vizuri”Massawe.
Akijibu risala ya wahitimu hao Mgeni rasmi Prof.Ndakidemi ametoa kiasi cha shilingi milioni mbili na kutaka uongozi wa taasisi hiyo kumpatia idadi na gharama ya vifaa hitajika ili kushirikiana na wadau wengine kufanikisha huku akimshukuru Mhisani Martin Massawe kwa kujitolea kusaidia upatikanaji wa kompyuta na vifaa vingine vya Tehama.
Kwa upande wake Mkuu wa taasisi hiyo Bi.Devotha Shayo amewataka wahitimu hao kutambua dhamana kubwa waliyo nayo katika kuhudumiajamii.
Jumla ya wahitimu 49 wamehitimu katika mafunzo ya kada ya afya ya kinywa na meno pamoja na wauguzi na ukunga huku wahitimu 7 wakishindwa kuhitimu kutokana na sababu mbalimbali.