Latest Posts

PROF. TIBAIJUKA AONYA TANZANIA KUTOCHUKUA SHERIA MKONONI KATIKA MZOZO NA MALAWI

Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania Profesa Anna Tibaijuka, ameonya kuwa hatua ya Tanzania kuzuia kwa upande mmoja usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini inaweza kuiweka nchi kwenye mgogoro mkubwa wa kimataifa kwa kukiuka mikataba ya kisheria inayolinda nchi zisizo na bandari.

Kupitia chapisho katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, Prof. Tibaijuka amesema Tanzania inaweza kulazimika kulipa faini au kuchukuliwa hatua za kisheria kimataifa kutokana na kile alichokiita “kulipiza kisasi kwa njia ya upande mmoja” (unilateral retaliation) nje ya utaratibu rasmi wa mashirika ya kikanda au kimataifa kama Shirika la Biashara Duniani (WTO) au Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

“Malawi ni nchi isiyo na bandari. Inalindwa na mikataba ya kimataifa inayotoa haki ya kupitisha bidhaa kupitia nchi jirani kama Tanzania bila ubaguzi wala vikwazo visivyo na msingi. Tanzania inaweza kupigwa faini kubwa kwa kuchukua sheria mkononi,” amesema Prof. Tibaijuka.

Ametaja mkataba wa WTO/GATT 1994, Ibara ya V, unaolinda uhuru wa usafirishaji (freedom of transit), ambao unakataza kuzuilia bidhaa za nchi zisizo na bandari bila sababu ya msingi. Pia ameeleza kuwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sheria ya Bahari (UNCLOS) unatoa haki hiyo kwa nguvu ya kisheria kupitia Ibara ya 125.

“Hatua za upande mmoja ni kinyume cha taratibu. Tanzania ilikuwa na wajibu wa kutumia mashauri ya WTO au SADC. Malawi inaweza kulalamika rasmi na kudai fidia,” amesema.

Prof. Tibaijuka, aliyewahi kuwa Mratibu Maalum wa Masuala ya Nchi Masikini, zisizo na bandari na visiwa vidogo (LDCs, LLDCs, SIDs) katika UNCTAD/WTO, amesema pia kuwa Tanzania haipaswi kupuuza mipango ya Umoja wa Mataifa kama Almaty Programme (2003) na Vienna Programme (2004) ambayo, japokuwa si sheria ya moja kwa moja, ina nguvu ya kisiasa na kidiplomasia katika kulinda nchi zisizo na bandari.

“Hatari ya hatua kama hizi ni kubwa. Tunaweza kusababisha madhara ya kidiplomasia na kiuchumi kwa taifa. Mazungumzo ni njia bora ya kumaliza mgogoro huu,” amesisitiza Profesa huyo.

Kauli ya Prof. Tibaijuka imekuja siku chache baada ya Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Mohamed Bashe, kutangaza hatua kali za kuzuia mazao ya kilimo kutoka Afrika Kusini na Malawi kuingia nchini, akisema hatua hiyo ni majibu kwa zuio lililotangazwa na nchi hizo dhidi ya bidhaa za kilimo kutoka Tanzania.

“Kuanzia usiku huu, Aprili 23, 2025, hautaruhusiwa zao lolote linalotoka Afrika Kusini kuingia nchini. Malawi hawajafuta notisi yao, hivyo natangaza rasmi marufuku kwa mazao yote ya kilimo kutoka Malawi kupita nchini kwetu,” alisema Bashe akiwa jijini Dodoma akibainisha kuwa uamuzi huo ni sehemu ya kulinda heshima ya biashara ya Tanzania, huku akiongeza kuwa hakuna Mtanzania atakayekufa kwa kukosa matunda kutoka Afrika Kusini kama tufaa (apples) au zabibu.

Waziri Bashe pia alisema kuwa hata mahindi ambayo yamenunuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa ajili ya msaada wa chakula kwa Malawi, hayataruhusiwa kupita nchini hadi pale soko la Tanzania litakapofunguliwa rasmi.

Aidha, alibainisha kuwa hata mbolea iliyopangwa kuchukuliwa Mei 1, 2025 kwa ajili ya msimu wa kilimo nchini Malawi haitaruhusiwa kutoka Tanzania hadi pale masharti ya usawa wa kibiashara yatakapotimizwa.

Waziri huyo alitoa kauli hiyo ikiwa ni utekelezaji wa onyo alilolitoa Aprili 17, 2025 kwa nchi hizo mbili kuondoa vikwazo kwa mazao ya Tanzania ndani ya siku saba, vinginevyo hatua kali zichukuliwe.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!