Na Helena Magabe, Tarime.
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeuhakikishia umma kuwa mifumo yake ya kidijitali ni salama, madhubuti, na imelenga kumaliza adha ya wastaafu kusafiri umbali mrefu kufuata huduma maofisini.
Uhakika huo umetolewa Januari 22, 2026, mkoani Mara wakati wa semina ya siku moja kwa waandishi wa habari iliyolenga kutoa uelewa wa huduma za PSSSF Portal na PSSSF Kiganjani, ambazo sasa ndizo nguzo kuu za utoaji huduma kwa wanachama na wastaafu.
Afisa Mahusiano Mwandamizi kutoka PSSSF Makao Makuu Dodoma, Rehema Mkamba, amesema mifumo hiyo inakaguliwa mara kwa mara ili kuhakikisha usalama wa taarifa za wanachama na wao wanalipa kwa wakati ili kuboresha ufanisi wa utendaji kazi kupitia mifumo hiyo ya kidijitali Mwanachama anajaza fomu ya mafao mtandaoni haitaji kuhangaika kwenda kuhakikiwa ofisini.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa PSSSF Mkoa wa Mara, Nuru Malinya, amefafanua kuwa huduma za kidijitali zimeongeza uwazi na ni mwarobaini wa utapeli uliokuwa ukiwakabili wastaafu huko nyuma. Amesema mifumo hiyo inamwezesha mstaafu kufanya uhakiki akiwa nyumbani kwake, jambo linalookoa muda na gharama za usafiri.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC), Mugini Jacob, ameupongeza mfuko huo kwa elimu hiyo na kushauri taasisi hiyo kuandaa tuzo maalum kwa waandishi wa habari ili kuwapa motisha ya kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha jamii kuhusu hifadhi ya jamii.
