Rais mpya wa Madagascar, Colonel Michael Randrianirina, ametangaza uteuzi wa Herintsalama Rajaonarivelo kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo, zikiwa ni siku chache baada ya jeshi kuchukua madaraka kufuatia kuondolewa madarakani kwa Rais wa zamani, Andry Rajoelina. Hatua hiyo inalenga kurejesha uongozi wa kiraia katika taifa hilo lililotumbukia katika mgogoro wa kisiasa wiki iliyopita.
Randrianirina, aliyekuwa akiongoza kitengo maalum cha jeshi (CAPSAT), alitangaza kuchukua madaraka baada ya bunge kumng’oa Rajoelina kwa kosa la kuzembea majukumu yake wakati wa maandamano ya wananchi waliokuwa wakipinga hali ngumu ya maisha na kukatika kwa umeme mara kwa mara. Aliapishwa kuwa Rais siku ya Ijumaa na kuahidi mageuzi makubwa pamoja na kuitisha uchaguzi huru.
Kupitia mashauriano na bunge, Rais Randrianirina alimchagua Rajaonarivelo, ambaye ni mfanyabiashara mashuhuri na mwenyekiti wa zamani wa benki ya BNI, kutokana na uzoefu wake na uhusiano wa kimataifa unaoweza kusaidia kuimarisha uchumi wa Madagascar. Alisisitiza kuwa uteuzi huo umezingatia Katiba na dhamira ya kujenga serikali shirikishi.
Katika hotuba yake, Randrianirina aliahidi kushirikiana na “nguvu zote za taifa” katika kuunda serikali ya kiraia itakayoweka kipaumbele katika utulivu wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi. Alikanusha madai kwamba jeshi lilifanya mapinduzi, akisisitiza kuwa hatua yao ilikuwa “kuokoa taifa dhidi ya uongozi ulioshindwa.”
Rais wa zamani Andry Rajoelina ameripotiwa kukimbilia kisiwa cha Réunion kupitia ndege ya kijeshi ya Ufaransa kabla ya kuelekea Dubai. Wafuasi wake wamepinga vikali hatua ya jeshi kuingilia mamlaka ya kiraia, wakisema ni jaribio jingine la kupindua serikali kama ilivyowahi kutokea katika historia ya taifa hilo.