Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameuagiza uongozi wa kiwanda cha Sukari Mkulazi kuhakikisha wanakisimamia vyema kiwanda hicho ili kiweze kuleta manufaa kwa Taifa.
Rais Samia ametoa maagizo hayo wakati wa akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho Wilayani Kilosa wakati akihitimisha ziara yake mkoani Morogoro ambapo amesisitiza kuishi kwa mradi huo wa kiwanda ili kuweza kuleta tija nchini.
“Nimepokelewa na kijana mmoja ambaye ndiye meneja wa mradi sasa basi hakikisha mradi huu unasimama usife, mradi huu ukifa na wewe unakufa”, ameeleza Dkt. Samia.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na biashara Dkt. Selemani Jafo amesema kuwa kiwanda cha sukari Mkulazi kinaenda kuondoa changamoto ya upungufu wa sukari nchini huku Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kiwanda cha sukari Mkulazi Dkt. Hildelitha Msita amesema kiwanda cha sukari Mkulazi kina uwezo wa kuzalisha tani elfu 50 kwa mwaka hivyo kiwanda hicho kina manufaa makubwa kwa Taifa
Naye mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema kuwa asilimia 70 ya sukari inayozalishwa nchini inatoka mkoa wa Morogoro hivyo kama mkoa utahakikisha wakulima wadogo wanazalisha miwa kwa ajili ya viwanda vya sukari mkoani humo.