Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameonesha kuridhishwa na kazi wanayoifanya askari wa polisi wa Tanzania katika kulinda amani na utulivu wa nchi huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Kupitia hotuba yake katika hafla ya kufunga Mkutano wa Mwaka wa Maofisa Wakuu wa Jeshi la Polisi, hafla ambayo pia iliadhimisha miaka 60 ya Jeshi hilo, Rais Samia amesema yapo mengi ya kujivunia kutokana na uwepo wa jeshi hilo hata hivyo akabainisha umuhimu wa kuendelea kuliboresha.
“Yapo mambo mengi ya kujivunia kwa Jeshi letu lakini pia yapo baadhi ya kuborehsa zaidi kama ilivyo bainishwa kwenye ripoti ya Tume ya Haki Jinai, ahadi yangu kwenu kama Amiri Jeshi Mkuu na Mkuu wa nchi ni kuendelea kuimarisha huduma za Polisi ili pamoja na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao huduma hizo pia zisaidie kuchochea ukuaji wa uchumi wetu na ustawi wa jamii kwa ujumla”, amesema Rais Samia.
Katika hotuba hiyo, Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania ni nchi yenye hadhi na kujitegemea, hivyo haiwezi kuamriwa na watu wa nje kuhusu jinsi ya kuendesha masuala yake ya ndani.
Amekemea vikali kauli za ‘kibaguzi’ kutoka kwa baadhi ya balozi wa kigeni baada ya kifo cha Ali Kibao, mwanachama wa CHADEMA. Rais Samia amefafanua kuwa kauli hizo hazikutolewa kwa ridhaa ya serikali za balozi hizo na alisisitiza umuhimu wa kuheshimu mamlaka ya Tanzania, kama vile balozi za Tanzania zinavyoheshimu mamlaka za nchi nyingine.
Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania haitaruhusu mataifa ya nje kuamua kwa niaba yake. Aidha, Rais alifichua njama zinazopangwa na “chama kimoja” cha upinzani, kilichofanya mkutano huko Arusha tarehe 11 Septemba, ambapo ajenda kuu aliitaja kuwa ya kutumia maandamano na vurugu kuvuruga serikali kwa matumaini ya kuipindua. Ameeleza kuwa hatua hizi ni hatari na zinaweza kuhatarisha usalama wa nchi.
Rais Samia pia alitoa wito kwa vyama vya siasa nchini kuheshimu falsafa yake ya 4R (Maridhiano, Uvumilivu, Haki, na Uwajibikaji) na kutumia uhuru wa kisiasa kwa busara. Amewakumbusha kuwa uhuru huo umepatikana kwa jitihada kubwa, na ni muhimu kuutumia kwa kuendeleza amani na utulivu, si kwa kuchochea kile alichokiita machafuko.