Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali inafanya mambo yake kwa mujibu wa mipango na siyo kuzuka kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakiikosoa kwa madai kuwa inanunua magari ya kifahari (V8) kwa ajili ya watendaji wake badala ya kununua matrekta kwa ajili ya wakulima.
Dkt. Samia, ameyasema hayo Alhamisi Agosti 8, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya sikukukuu ya wakulima kitaifa Nanenane iliyofanyika katika viwanja vya Nzuguni.
“Nimekua nikisikia watu wanasema serikali inafuja fedha kwa kununua magari kwa ajili ya watendaji wake badala ya kununua matrekta kwa ajili ya wakulima, ndugu zangu serikali inafanya mambo yake kwa kuzingatia mipango yake haizuki tu, bila kununua magari ya watendaji tunayofanya yote ni bure nani atakwenda kusimamia?”, amesema Rais Dkt. Samia.
Amesema, lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo 2030 serikali inapeleka matrekta 10,000 pamoja na Powertiller 10,000 kwa wakulima.
“Vile vile serikali imeimarisha hivi sasa huduma za ugani pamoja na vitendea kazi na sisi serikali tumejenga maabara bora ya kilimo ambayo sampuli zote zitakuwa zinapita pale ifikapo mwaka 2026”, amesema.
Kwa upande Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, amesema Ilani ya uchaguzi ya CCM inaitaka wizara hiyo ifikapo 2025/26 sekta hiyo iwe imefikia asilimia 130.
Aidha, amesema katika mauzo yatokanayo na mazao ya kilimo wamepanga kufikia Dola za Kimarekani bilioni 2.6 mwaka huu kutoka mauzo ya dola za Kimarekani bilioni 2.3 za mwaka jana.
Hata hivyo amesema kutokana na utaratibu wa serikali kutoa ruzuku ya mbolea kumesaidia kuongeza matumizi kutoka tani 360,000 hadi tani 900,000.
Kadhalika, amesema wizara yake inakwenda kuwatoa watu wote walivamia maeneo ya serikali hususani yale ya kilimo.
“Mheshimiwa Rais tunakwenda kuwatoa wote waliovamia maeneo ya serikali hususani yale ya kilimo ya TARI na Nanene kwani uvamizi wa maeneo ya serikali umefika mwisho”, amesema.